Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sudan Kusini kukabidhiwa uenyekiti EAC kesho

Eac Sudan.jpeg Sudan Kusini kukabidhiwa uenyekiti EAC kesho

Wed, 22 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkutano wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), unatarajiwa kuanza kesho Alhamisi Novemba 23, 2023 jijini Arusha ukiwakutanisha pamoja marais au wawakilishi wao kujadili masuala mbalimbali.

Mkutano huo wa siku mbili, utajadili suala la usalama wa chakula ndani ya jumuiya katika siku ya kwanza, na siku ya pili, Ijumaa Novemba 24, 2023, watachagua Mwenyekiti mpya wa EAC.

Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye anatarajiwa kukabidhi uenyekiti wa EAC kwa Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir. Hiyo itakuwa ni mara ya kwanza kwa Taifa hilo kuongoza EAC tangu ilipojiunga mwaka 2016.

EAC inayoundwa na nchi saba wanachama, imekuwa na utaratibu wa kupokezana nafasi ya uenyekiti kila baada ya mwaka mmoja kwa kufuata mzunguko. Sasa ni zamu ya Taifa changa la Sudan Kusini lililoanzishwa Julai 2011.

Jumuiya imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya baadhi ya nchi wanachama kutolipa ada zao za uanachama kwa wakati, na mataifa yaliyokuwa yanaongoza kutolipa ni Sudan Kusini na Burundi.

Hata hivyo, Sudan Kusini ilitangaza kukamilisha malipo ya malimbikizo ya madeni yake hivi karibuni, ambayo jumla ya Dola za Marekani 7 milioni (Sh17.528 bilioni) zikiwa zimebaki siku chache kutwaa uenyekiti wa jumuiya hiyo.

Wakati mkutano huo ukisubiriwa, tayari mikutano mingine imekuwa ikiendelea kufanyika katika ofisi za makao makuu ya EAC, na jana Jumanne kilifanyika kikao cha Baraza la Mawaziri wa nchi wanachama ambalo lina wajibika moja kwa moja kwenye mkutano wa viongozi.

Wakizungumzia hatua ya Sudan Kusini kutwaa uenyekiti wa EAC, wachambuzi wa masuala ya siasa na diplomasia wamebainisha kazi iliyo mbele ya Taifa hilo na mambo inayotakiwa kuyafanya katika uongozi wake.

Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia cha Salim Ahmed Salim, Innocent Shoo ameipongeza Sudan Kusini kwa kukamilisha malipo ya malimbikizo ya madeni yake ya ada na kuitaka kwenda kusimamia jambo hilo, kuhakikisha wanachama wanalipa ada zao kwa wakati.

Amesema Sudan Kusini kama mwenyekiti, inatakiwa kuhakikisha amani inaendelea kuwepo kwa kuwa nchi za Afrika Mashariki, wakiwemo wanachama wawili, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Sudan Kusini yenyewe zinakabiliwa na vita.

Shoo amesema nchi jirani zinazopakana na EAC kama vile Ethiopia, Somalia, Msumbiji zinakabiliwa na mapigano ya mara kwa mara, jambo linalohitaji usimamizi na mikakati ya kuhakikisha amani inakuwepo.

“Kwa hiyo, usalama usimamiwe vizuri, lakini pia uchangiaji wa ada za uanachama uwe wa uhakika ili kusukuma nguzo za jumuiya. EAC inapokuwa haina bajeti ya kutosha, inakuwa vigumu kutekeleza mipango yake,” amesema.

Ameongeza ni muhimu Sudan Kusini ikaendelea kuondoa vikwazo vya watu kusafiri sambamba na kusafirisha bidhaa ndani ya jumuiya, ili kuongeza mwingiliano utakaokuza biashara na shughuli za kiuchumi. “Misingi ya kidemokrasia iendelee kulindwa kama ilivyokuwa Liberia, Rais George Weah kukubali kushindwa na anaondoka kwa amani. Maana yake ni kwamba chaguzi ziwe huru na haki ili tusihatarishe amani,” amesema Shoo.

Kwa upande wake, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulie amesema Sudan Kusini waanze kujiweka sawa wenyewe ndani kwa sababu itaweza kuwa na ushawishi katika kuongoza wengine.

“Lazima waanze kuweka sawa mambo yao ya ndani. Unajua Sudan Kusini kuna majibizano na sintofahamu kati ya Serikali na wapinzani au wale wanaoipinga Serikali. Hilo litawasaidia kuaminika na kuwa na ushawishi,” amesema.

Dk Loisulie amesema Sudan Kusini ina kazi kubwa ya kuonyesha kwamba hata kama ni taifa changa, linaweza kuwa na ushawishi na kuweza kusukuma gurudumu la kidiplomasia katika nchi nyingine.

“Ni muhimu Rais na watu wake waonyeshe uwezo. Bahati nzuri kuna kanuni na miongozo ya uendeshaji wa jumuiya, ziko wazi. Lakini uwepo wa kanuni peke yake hautoshi, lazima waje kuonyesha kitu kipya ambacho wengine hawakufanya,” amesema.

Mwanazuoni huyo ameongeza, Sudan Kusini itumie kiti hicho kutatua matatizo yake ya ndani hasa kuondoa vikwazo kwenye usafirishaji wa chakula kutoka kwa nchi moja mwanachama kwenda nyingine.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live