Hadi kufikia sasa hospitali na vituo vingi vya matibabu katika mji mkuu wa Sudan Khartoum vimeshambuliwa kwa makombora katika mapigano yaliyozuka Aprili 15 kati ya majenerali hasimu na vikosi wanavyoviongoza.
Umoja wa Mataifa umeeleza kuwa, kufuatia mapigano hayo, ni asilimia 16 pekee ya hospitali mjini Khartoum ndizo zinafanya kazi kikamilifu, hali inayoyaweka maisha ya watu wengi hatarini. Hata hivyo hospitali ndogo ya Al-Nada iliyoko katika mji pacha wa Omdurman wa Khartoum imesalia kuwa kituo cha kuokoa maisha ya wagonjwa;ambapo imeacha milango yake wazi ikiendelea kutoa huduma muhimu za afya kwa wagonjwa mbalimbali hasa akina mama wajawazito licha ya kuendelea mapigano na hali ya mchafukoge.
Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa kuna wanawake wajawazito 219,000 huko Khartoum wakiwemo elfu 24 wanaotazamia kujifungua katika wiki chache zijazo.
Hospitali ya Al-Nada inategemewa pakubwa kuwahudumia akina mama hao wajawazito. Mohammed Fattah al-Rahman Mkurugenzi wa hospitali ya Al-Nada huko Khartoum ameeleza kuwa: Hadi sasa wameweza kutoa huduma kwa akina mama wajawazito ambapo wamewazalisha watoto 500, kwa njia ya kawaida na kwa njia ya upasuaji, na wakati huo huo kulaza watoto wengine 80 wenye matatizo mbalimbali".
Amesema wanakabiliwa na hali ngumu kwa sababu hakuna viyoyozi katika hospitali hiyo, ni feni za juu tu ambazo hujaribu kupunguza joto ambalo mara nyingi hufikia hadi nyuzi joto 40 hata kabla ya kilele cha msimu wa joto kali.