Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula ameamuru kwamba wabunge wa Azimio la Umoja One-Kenya ambao walipokonywa walinzi warejeshewe.
Hii ni baada ya wabunge wapatao 22 wa mrengo huo wa upinzani, Alhamisi alasiri, kulalamika kuwa walipokonywa walinzi kinyume cha sheria za bunge na sheria zingine husika.
“Serikali haifai kuendelea kuwatisha wabunge wa upinzani kila mara kwa kuwapokonya walinzi ilhali ni haki yao kupata huduma hiyo kwa gharama ya umma,” akafoka Mbunge Maalum John Mbadi.
Akiunga mkono kauli hiyo, Mbunge wa Nyando Jared Okello alisema ni haki ya kikatiba ya wabunge wote kupata huduma za walinzi ambao ni maafisa wa polisi kila mara.
“Ni haki ya wabunge 349 na maseneta 67 kupewa ulinzi bila kuegemea mrengo wao wa kisiasa. Huduma hii inapasa kugharamiwa na Tume ya Huduma za Bunge (PSC),” akasema Bw Okello (mbunge wa ODM).
Suala hilo liliibua mjadala mkali bunge wakati wa kikao cha alasiri, huku kiongozi wa wengi Kimani Ichung’wa akiwalaumu wabunge wa upinzani kwa “kutumia vibaya walinzi wao haswa nyakati za maandamano.”
“Nitaongea na Waziri wa Usalama na Inspekta Jenerali wa Polisi kuhusu suala hili. Ikibainika kuwa kuna wabunge ambao walinzi wao wameondolewa, nitaomba warejeshewe. Lakini nasisitiza kuwa tukome kuwatumia vibaya maafisa wetu,” akasema Bw Ichung’wa, ambaye ni Mbunge wa Kikuyu.
“Ikiwa unataka kwenda katika maandamano, enda kivyako. Usiwalazimishe maafisa wa polisi uliopewa kama walinzi kukufuata. Ikiwa unataka kuenda katika shughuli zako za kibinafsi, waruhusu maafisa wako waende nyumbani,” akaongeza.
Bw Ichung’wa alisema wabunge wa Azimio walipokonywa walinzi kwa sababu walikuwa wakiwatumia vibaya maafisa wa polisi waliopewa na serikali kuwalinda.
“Katika mazingira kama hayo ya maandamano, maafisa hawa wanaweza kulazimika kutumia bunduki zao visivyo,” akasema Ichung’wa.
Hata hivyo, madai hayo yalipingwa na wabunge wa upinzani waliosema serikali inacheza siasa na usalama wao.
“Kisheria, Makamu wa Rais wa zamani na Waziri Mkuu wa zamani wanapaswa kupewa ulinzi. Wabunge pia wanapasa kupewa walinzi. Hii ni sheria na serikali haina mamlaka ya kuibadili bila kurejeshwa kwetu katika bunge hili,” akasema Mbunge wa Rarieda Otiende Amollo.
Mnamo Jumatano, vinara wa Azimio waliisuta serikali kwa kuwapokonya walinzi ili kusambaratisha mipango yao wa kushiriki maandamano jijini Nairobi.