Serikali ya Somalia imetoa amri kwa makampuni ya mawasiliano ya simu, benki za kuhamisha fedha na mashirika mengine ya biashara kusajili biashara na wateja wao kwa mamlaka ili kuzuia utoroshaji wa pesa na ufadhili wa ugaidi, TV ya Taifa ya Somalia inayomilikiwa na serikali imeripoti.
Katika mkutano na wanahabari siku ya Jumanne, Waziri wa Habari Daud Aweis pia aliwataka watoa huduma za simu kusajili wateja na kukusanya maelezo yao binafsi ikiwa ni pamoja na alama za vidole na picha.
Waziri huyo alisema Kamati ya kitaifa ya Serikali ya kupambana na utakatishaji fedha na kukabiliana na ufadhili wa ugaidi pia imetoa angalizo kwa umma dhidi ya kusaidia wanamgambo.
"Umma unaombwa kuepuka hatua zozote zinazoweza kusaidia ugaidi haswa uhalifu wa utakatishaji fedha na ufadhili wa ugaidi, ambao ni vitendo vikuu vya uhalifu," Bw Aweis alisema.
Aliwataka wafanyabiashara wote kujisajili na kuonya kuwa biashara au mali yoyote itakayopatikana inahusishwa na wanamgambo hao itakamatwa.
Waziri huyo aliongeza kuwa leseni zitafutiliwa mbali kwa kampuni yoyote itakayokiuka maagizo ya serikali.
Alisema hatua hiyo inalenga kupunguza vyanzo vya mapato ya wanamgambo na kuzuia ufujaji wa fedha unaohusiana na ugaidi.
Siku ya Jumanne, shirika hilo la upelelezi lilionya wafanyabiashara dhidi ya kusafiri katika maeneo yanayodhibitiwa na al-Shabab kuitikia wito wa kundi hilo la wanamgambo.