Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Soka linavyoathiriwa na imani za ushirikina

89200 Ushirikina+pic Soka linavyoathiriwa na imani za ushirikina

Fri, 20 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

MEDANI ya michezo katika nchi nyingi, pamoja na Tanzania, imeshindwa kupiga hatua kwa miaka nenda rudi kutokana na wachezaji na vongozi kutumia muda mwingi na pesa katika mambo ya ushirikina badala ya mazoezi, ambayo ndiyo msingi wa mafanikio.

Timu zinazofanya mambo ya ushirikina huamini zinaweza kuwadhoofisha wachezaji wa upinzani na hata waamuzi ili zipate ushindi. Kwao wao ushindi ni muhimu kwa gharama yoyote ile, hata ikiwa ni pamoja na kuuwa watu ndani au nje ya viwanja.

Wakati mwingine hufanyika kwa watoto wadogo wasiokuwa na hatia kwa maelezo ya ati walitolewa kafara. Hii ni laana isiyoweza kukubalika.

Ushirikina hugharimu fedha nyingi ambazo zingesaidia kuimarisha timu badala ya kutumika kwa mchezo huu mchafu.

Yapo matukio yaliyohusishwa na ushirikina katika nchi mbali mbali yaliyosababisha maafa makubwa. Kwa mfano, tarehe 29 Oktoba, 1998 katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo wachezaji wote 11 wa klabu ya Bena Tshadi wenye umri wa kati ya miaka 20 na 35 waliokuwapo uwanjani walikufa wakati mmoja baada ya kupigwa na radi.

Lakini hata mchezaji mmoja wa klabu ya Bisanga waliocheza nayo katika uwanja wa nyumbani kwao katika jimbo la Kasai hakupata mkwaruzo.

Radi ilipiga wakati matokeo ya mchezo yakiwa 1-1 na wachezaji wa timu hizo mbili walikuwa wamechanganyika na sio kwamba walikuwa kila timu ipo upande wake wa uwanja.

Kilichosikitisha ni kwamba maafa hayo yalihusishwa na mambo ya ushirikina ambayo yanapendwa sana katika jimbo hilo la Congo ambalo kwa muda mrefu sasa lipo katika mapigano.

Hii ilisababisha klabu nyingi kukataa kucheza na Basanga kwa kuhofia maafa yaliyohusishwa na ushirikina.

Maafa haya ya Congo yalitokea siku chache baada ya radi kupiga katika mchezo wa Ligi Kuu ya Afrika ya Kusini katika pambano la Moroka Swallows na Jomo Cosmos uliofanyika Johannesburg. Wachezaji saba na muamuzi walizimia uwanjani.

Ikadaiwa kwamba wataalamu wa ushirikina wa Kasai walikwenda Afrika ya Kusini kufanya vitu vyao katika mchezo ule.

Katika miaka ya 1970 wachezaji wa klabu moja ya Afrika ya Magharibi iliyosifika kwa ushirikina waliomba wasiendelee na mchezo muda mfupi tu baada ya kuanza katika uwanja wa Kinshasa.

Wachezaji hao walilalamika kuona kizunguzungu na kupoteza nuru ya macho.

Watanzania tumeshuhudia mara kwa mara baadhi ya klabu zikijihusisha na jambo hili, na mara kadhaa klabu za nchini, zikiwamo Simba na Yanga, zimepigwa faini kwa kufanya matukio tata yanayohusishwa na imani za ushirikina.

Mambo haya yapo kwenye ligi za mchangani hadi katika timu ya taifa.

Ninakumbuka Taifa Stars ilipokwenda kucheza dhidi ya Ethiopia mwanzoni mwa miaka ya 1980 ilifuatana na wachawi waliopewa jina la kamati ya ufundi.

Hawa walikuwa wazee watatu ambao waliwapa wachezaji wetu hirizi na kuwachanja kwenye mapaja na tulifungwa 1-0.

Timu iliporudi Dar es Salaam wachezaji walilamikia maumivu ya chanjo na kufungwa hirizi kubwa ambazo ziliwasumbua walipokuwa wanakimbia.

Kamati ya ufundi ilivunjwa na wachezaji waliofikia Hoteli ya Mawenzi (sasa Holiday Inn, Barabara ya Maktaba) waliingia Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kwa mchezo wa marudiano bila ya hirizi wala mzizi au chanjo na timu yetu kuibuka na ushindi wa 3-0.

Mabao yote yalifungwa na marehemu Jumanne Masimenti aliyekuwa anachezea timu ya Cosmo ya Dar es salaam.

Mara nyingi tumeona katika michezo yetu, ikiwa pamoja na katika Ligi Kuu, yakivunjwa mayai viza uwanjani kabla ya mchezo kuanza au golikipa kukuta kichwa cha njiwa golini.

Ni vizuri tukawa na sheria kali zitazoonyesha ushirikina haupewi nafasi sio kustawi, lakini hata pia kuchomoza katika michezo nchini.

Klabu zinazohusika na mchezo mchafu zifungiwe kwamuda mrefu au kuteremshwa daraja.

Tusijidanganye. ushirikina hauleti ushindi katika mchezo na kama unasaidia siku zote Haiti ingeliibuka kidedea.

Katika fainali za Kombe la Dunia za 1974 zilizofanyika Magharibi Haiti ilikwenda na wachawi zaidi ya 50, wanaume na wanawake.

Badala ya kufanya vizuri ilirudi nyumbani na kikapu cha magoli ya kufungwa. Katika mchezo wao wa kwanza walichapwa 3-1 na Ufaransa, baadaye wakafungwa 7-0 na Poland na walifungishwa virago kwa kuchapwa 4-1 na Argentina.

Afrika Kusini katika fainali za Kombe la Dunia 2010, waganga (masangoma) walifanya matambiko katika viwanja vyote na wakatamba timu yao Bafana Bafana itatwaa ubingwa. Ikatolewa hatua ya makundi.

Michezo ni burudani ambayo lengo lake kubwa ni kuleta raha na furaha kwa jamii na kujenga urafiki na maelewano na sio maafa.

Chanzo: mwananchi.co.tz