Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Siri ya familia ya Kenyatta yafichuliwa

KenyattaA0024 Siri ya familia ya Kenyatta yafichuliwa

Sun, 10 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mzee Jomo Kenyatta, rais wa kwanza wa Kenya alifariki saa chache kabla ya kukutana na aliyekuwa hasimu wake mkuu wa kisiasa, Jaramongi Oginga Odinga wazike tofauti zao.

Haya yamefichuliwa na aliyekuwa Mbunge wa Dagoretti Beth Mugo, mpwa wa Jomo Kenyatta na rafiki wa karibu wa muda mrefu wa Mama Ngina Kenyatta, Mama Taifa wa Kwanza wa Kenya.

Katika kitabu kuhusu maisha yake ‘Early Bird’, Bi Mugo anasimulia kwamba kaka yake, Ngengi Muigai na Mzee Kenyatta walikuwa wamepanga mkutano wa upatanisho na Jaramogi.

“Kwa hakika, Mzee Kenyatta alikuwa akipanga na kaka yangu, Ngengi Muigai, kukutana na Jaramogi kwa maridhiano. Mkutano wa kukutana na Mzee ulikuwa umeahirishwa mara mbili kwa sababu ya shughuli nyingi za rais.

"Kwa bahati mbaya, Mzee alikufa Agosti 22, 1978, saa chache kabla ya mkutano uliopaswa kufanyika Agosti 23, 1978, katika Ikulu ya Mombasa. Ngengi, aliyekuwa Nairobi kumchukua Jaramogi na timu yake alilazimika kusafiri Mombasa usiku huo baada ya kupata habari kwamba Mzee Kenyatta alikuwa amekufa,” Bi Mugo anaeleza.

Anasema Jaramogi alidondokwa na machozi alipotazama mwili wa Mzee Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi akilia kuwa “siamini rafiki yangu Kenyatta amekufa”.

Katika kitabu hicho, Bi Mugo anafichua maisha ya dhiki ya familia ya Kenyatta na masaibu iliyopitia ikiwemo kutoweka kwa kaka yao Kungu Muigai akiwa na umri wa miaka 13.

“Inaaminika alitafunwa na wanyamapori,” anaandika.

Anaeleza kuwa katika utawala wake wa miaka 16, Mzee Kenyatta alisafiri nje ya nchi mara moja tu alipohudhuria kutawazwa kwa Haile Sellasie kuwa kiongozi wa Ethiopia.

Bi. Mugo anasimulia kwamba Mzee Kenyatta alikamatwa na serikali ya wakoloni 1952, mwaka mmoja baada ya kumuoa Mama Ngina.

Baada ya kuachiliwa kutoka kizuizini, kitu cha kwanza ambacho Mzee Kenyatta alifanya ilikuwa ni kualika waliomsaliti kwa wakoloni nyumbani kwake, wakala nyama na kuzika tofauti zao na kuungana “kuwaandaa Waafrika kwa uhuru.”

Chanzo: www.tanzaniaweb.live