Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simulizi ya mwanamke aliyebakwa na mpenzi wa mama yake akiwa mtoto

Evelyine Simulizi ya mwanamke aliyebakwa na mpenzi wa mama yake akiwa mtoto

Wed, 15 Jul 2020 Chanzo: BBC

Kila mara Evalyne Mumbi anapowaza kuhusu maisha yake ya utotoni huwa haamini ni vipi aliweza kuepuka kifo cha mapema, kutokana na masaibu aliyoyapitia.

Evalyne anakumbuka siku moja asubuhi mapema alipobakwa akiwa msichana mdogo.

''Nakumbuka uzito na harufu iliyokuwa inatoka mdomoni mwa mwanamume alivyokua amenikosesha pumzi asubuhi ile kutokana na unyama alionitendea nikiwa mtoto wa miaka 7'', anasema Evalyne.

Evalyne anakumbuka mwanamume huyo akinong'ona na kumtishia.

"Alichonifanyia mama yako, nami pia nitalipiza kwako, mama yako amefanikiwa kuniachia ugonjwa wa Ukimwi nami pia nitakupatia kwa nguvu, sote tutalia, sote tutakufa," Evalyne anamkumbuka mwanamume huyo akisema.

Evalyne alikuwa bado ni bikira. Hakuamini kuwa alipokonywa ubikira wake na mwanamume aliyekuwa na machungu kutokana na uhusiano wake na mama yake mzazi. Evalyne alipoteza fahamu wakati alipobakwa na aliyekua mpenzi wa mama yake

Evalyne alipoteza fahamu wakati akitendewa unyama huo.

Ni tukio ambalo humtoa machozi kila mara anapolikumbuka, kwani walipotoka nyumbani siku hio, Mumbi alikuwa amefahamishwa na mama yake kuwa walikuwa wanakwenda kumtembelea shangazi yake aliyekuwa anaishi mtaa wa kifahari.

Mumbi alikuwa anapenda sana kutembea na mamake hususan alipojua kuwa walikuwa wanamtembelea jamaa wao aliyekua akiishi maisha ya kifahari.

Anasema wakali walipoanza safari, mama yake alibadilisha wazo na kumweleza kuwa alikuwa akutane na rafiki yake.

''Akilini nilidhani tu ni rafiki wa kike ila tulipofika katika nyumba ya rafiki huyo niligundua kwamba alikuwa ni mwanaume'', anasema. Usiku wa kiza Evalyne Wanja alibakwa alipokuwa na mama yake katika nyumba ya mwanaume

Siku hiyo walilala nyumbani kwa mwanamume huyo.

Mumbi anakumbuka kuwa mama yake na mpenzi wake walilala kwenye kitanda kimoja naye akalala sakafuni.

Mumbi anasema kuwa katika umri wake anakumbuka akipata usingizi mzito hadi asubuhi.

"Ni sauti ya mlango ukifunguliwa iliyonizindua kutoka usingizini. Mama alinieleza amekwenda dukani kununua maziwa ili apike chai. Lakini pindi mama alipoondoka yule mpenzi wake alianza kuniita na kuniuliza iwapo nimelala. Ghafla alinirukia na kuanza kunibaka," Mumbi anasema.

Mama alirejea na kukuta nikiwa nimezimia huku damu ikiwa imetapakaa kwenye shuka.

Mama yake na mpenzi wake walijibizana na Wanja anakumbuka mama akimuuliza mwanamume huyo ni: ''kwanini umeamua kuharibu mtoto mdogo?.''

''Mwanamume huyo alikuwa akirudia tu kwamba ni lazima mama yangu ajute''. anakumbuka

Mumbi anakumbuka mama yake alimbeba na kumkimbiza nyumbani kwa mwanamke mmoja ambaye katika utu uzima huu Wanja hudhani alikuwa ni muuguzi kwani alizishona sehemu zake za siri zilizokuwa zimeraruka wakati wa ubakaji na pia akampatia dawa ameze.

Baadaye Mumbi na mama yake walianza safari ya kurejea nyumbani kwao, ila Mumbi anakumbuka kuwa mama yake alimuonya asithubutu kusema yaliyomtokea.

Kibaya zaidi ni kuwa Mumbi alikuwa anahisi uchungu mno na maswali mengi yalikuwa yakimjia akilini kuhusu ni kwa nini hawakwenda kupiga ripoti kwa polisi.

"Mama yangu alinionya dhidi ya kumueleza bibi kilichojiri. Pia niliogopa hasira ya mama yangu kwa hivyo nilinyamaza huku nikiuguza majeraha ya ubakaji kimya kimya," anakumbuka.

"Mama alikuwa akiniuguza na kunipangusa na kitambaa kilichokuwa na maji na chumvi katika sehemu zangu za siri kwa wiki kadhaa."

Ilimbidi Mumbi ajilazimishe kusahau kisa hicho, ila anasema kilimfanya awaogope sana wanaume.

Ni kisa ambacho kilimsumbua sana, ila kwa kuwa alikuwa bado msichana mdogo hakuwa na la kufanya ila kusahau tukio hilo.

Ilikuwa mara ya mwisho kwake kumuona mwanaume aliyemtendea unyama huo, na anafikiri uhusiano kati yake na mama yake ulifikia kikomo.

Dhiki utotoni

Malezi Evalyne Mumbi ya kimsingi akiwa mtoto yalikuwa mikononi mwa bibi (nyanya)yake

Evalyne Mumbi, anasema kuwa alizaliwa katika mazingira ambayo mama yake mzazi hakuwa katika ndoa.

Alijipata akiwa katika malezi ya bibi wakati mwingi. Mama yake alikuwa bado mdogo kwa umri na wakati mwingi hakuwa nyumbani.

"Nakumbuka mama yangu alikuwa mwanamke mwenye kupenda kutembea sana. Alikuwa anasafiri wakati mwingine kwa wiki kadhaa bila kuonekana nyumbani. Akirejea, angekaa nami kwa muda mfupi na kisha kutokomea," Evalyne anasema.

Kwahivyo malezi yake ya kimsingi akiwa mtoto yalikuwa mikononi mwa bibi, ila alitamani sana malezi ya upendo wa mama yake, vitu ambavyo hakuvipata.

Mumbi anasema kuwa ni maswali ambayo alizidi kumuuliza mama yake kila alipopata nafasi.

"Nilikuwa namuuliza mama yangu mzazi maswali mawili, la kwanza ni kwa nini wewe huniacha na kwenda siku nyingi bila kuonekana? La pili nilimuuliza, je mama wewe huenda wapi kila wakati haupo nyumbani?" anasema.

Ila wakati mwingi hakupata majibu ya maswali hayo, kwani mama yake alipokuwa anarejea kutoka alikokuwa anakwenda alikuwa ni mwingi wa mapenzi, na alikuwa anarejea na zawadi nyingi pengine katika hali ya kumpumbaza Mumbi.

Au labda ilikuwa tu njia rahisi ya kuepuka kujibu maswali hayo, anasema.

Mumbi anasema kuwa alikuwa anampenda sana mama yake, lakini hawakuwa na wakati mwingi pamoja.

Mumbi anakumbuka kuwa mama yake alikuwa mtu msafi mno, na kwa hivyo aliporejea alikuwa anamuosha nywele, na kumvisha nguo safi, kumchana nywele zake na kuwa binti aliyependeza sana.

Hatahivyo, akiondoka tu bibi hakuwa na muda wa kudumisha kiwango hicho cha usafi.

Maisha yaliendelea hivyo kwa miaka mingi hadi pale siku moja ghafla mama yake aliporejea nyumbani na kuonekana kama mgonjwa. Baada ya kuugua mama yake Evalyne alianza kumchapa na kumkaripia bila sababu

Kwa kuwa walikuwa wanaishi katika mazingira ya kijijini, uvumi ulienea kuwa mama yake alikuwa anaugua ugonjwa wa Ukimwi.

Ulikuwa uvumi kwahivyo hilo halikumsumbua Mumbi wakati huo.

Ni wakati huo pia ambapo mama yake alibadilika sana, sauti nyororo na ya upendo iligeuka na kuwa ya ukali na machungu mno.

Mama aliyekuwa kipenzi chake akaanza kumchapa kwa makosa madogo madogo ambayo hayakustahili kichapo

Msiba mara mbili

Wakati huo Mamake aliporejea nyumbani alikuwa na ujauzito. Alipojifungua mtoto wa kiume Mumbi alijifunza kumpenda nduguye, ila nduguye alikuwa anaugua kila wakati.

Baada ya muda wa miezi 6 aliaga dunia. Ni hali ambayo ilimwathiri Wanja na zaidi mama yake mzazi kwa kiasi kuwa alizidi kuonyesha ishara za mwanamke aliyekuwa anapitia hali ngumu .

Wanja anakumbuka kuwa mamake alishika ujauzito wa pili na kujifungua mtoto wa kiume tena.

"Nakumbuka kuwa ndugu yangu alikuwa mtoto wa kutabasamu na furaha. Mama alifanya kila awezalo kumlinda mtoto na kwa hivyo katika miezi yake ya kwanza alihakikisha kuwa alikuwa anampeleka kliniki kupata chanjo za kawaida... La kushangaza ni kuwa mama alitaka sana niandamane naye katika shughuli ya kliniki," Mumbi anasema

Ila Mumbi anasema kuwa mama yake alikuwa na tabia ya kutoingia na mtoto wake hospitalini.

Alikuwa anawalipa wanawake tofauti ili waandamane na mtoto na Mumbi , huku mama akisalia kwenye lango kuu la kuingia hospitalini.

Siku mmoja wanja anasema kuwa walipoandamana na mama mwingine aliyelipwa na mama yake kumpeleka mtoto kupata chanjo, Muuguzi alisisitiza kuwa mama afanyiwe uchunguzi kwa kuwa mtoto yule alipatikana na virus vya HIV wakati wa chanjo...Kwa hivyo ilibidi mama mzazi awepo.

Wakati huo ndipo Mumbi alipogundua kuhusu siri ya mamake, kwa kuwa alikuwa bado msichana mdogo na pia kwa kumuogopa mama, Wanja aliamua kutoligusia suala hilo, ila katika umri aliokuwa nao alikuwa ameelewa kuwa ugonjwa wa Ukimwi ulikuwa unasababisha kifo.

Haikuchukua muda pia kwa ndugu yakeWanja akafariki akiwa na umri wa mwaka mmoja.

Baada ya hapo Mumbi anakumbuka kuwa mama alibadilika sana. Mama alianza kumuadhibu hata zaidi na kumlaumu kwa matukio ya maisha yake.

"Mama yangu alikuwa ananifinyafinya mno usiku wakati nimelala hadi kunitoa damu, pia alikuwa akitemea chakula changu mate. Wakati mwingine mate haya yalikuwa na damu. Sikuwahi kuelewa kwa nini mama alikuwa ananitesa hivyo ila kwa yote mimi niliendelea kumpenda."

Hali ya afya ya mama yake pia ilidhoofika.

Katika mazingira hayo Mumbi naye alianza kuugua ugonjwa wa vidonda vya tumbo kwa kuwa alikuwa anahisi kana kwamba hakupendwa na mama yake.

Wanja pia alitamanani mno kumfahamu babake mzazi. Mamake alikuwa anamuelezea hapa na pale kuhusu baba yake kwa mfano jina lake, sehemu alikoishi na hata kumuonyesha picha yake, ni picha aliyoihifadhi na kuienzi kwa miaka mingi .

Kifo cha Mamake

Mama alizidi kuugua mara kwa mara na akawa mtu ambaye hangetoka nje kwa urahisi. Mumbi anakumbuka kuwa muda mwingi mama yake alisalia chumbani akiwa mpweke na kudhoofika asiweze hata kwenda msalani.

Mumbi anasema kuwa ni yeye aliyekuwa anazifua zile nguo na hata kutupa na kumwaga uchafu wa ndani sana wa mama yake.

Mwishowe alifariki dunia alipokua njiani kupelekwa hospitalini.

Mama yangu alikuwa amekataa kumeza dawa za kupunguza makali ya virusi vya HIV, na kwa hivyo alipoaga dunia, kijiji kizima kilifahamu kilichosababisha kifo chake'', anasema Mumbi.

Licha ya kwamba Mumbi alipitia mateso mengi sana mikononi mwa mama yake, tukio la kifo cha mama yake , lilimuachia majonzo makubwa. Kunusurika dhidi ya virusi

Ni wakati huo ambapo Mumbi alianza kumtafuta baba yake mzazi, alikumbuka maongezi ya mama yake kuhusu alikokuwa baba yake hadi akampata.

Wanja anakumbuka kuwa baba yake mzazi alimpokea vyema na hadi sasa bado wanaendelea kufahamiana zaidi.

Mumbi alipofikia utu uzima alikutana na mpenzi wake, ambaye kwa kwa sasa ni mume wake wa zaidi ya miaka minane.

Safari ya ndoa ilianza kwa changamoto, kwani kulingana na Mumbi, mwili wake ulidhoofishwa na magonjwa mbalimbali ikiwemo saratani.

Cha ajabu ni kuwa ule ubakaji ambao ulifanyika akiwa msichana mdogo haukumsababisha yeye kupatwa na virusi vya HIV.

Ni jambo ambalo limemsukuma sana katika taaluma yake ya uandishi wa vitabu. Mumbi amelenga sana uandishi kuhusu msamaha, kuhusu kuelewa matukio yenye changamoto katika maisha na pia huelekeza nguvu kuwahamasisha watu kuzungumza na wazazi na aina ya malezi yanayotolewa kwa watoto. Wanja ameandika vitabu viwili kwa sasa juu ya mahusiano ya wazazi na watoto wao

Wanja ameandika vitabu viwili kwa sasa juu ya mahusiano ya wazazi na watoto wao

Mumbi anasisitiza kuwa mzazi mwenye machungu, mzazi mwenye majuto ya maisha yake ana urahisi wa kumtupia mtoto au watoto wake kero ambazo sio makosa yao

Kwa hivyo anatoa changamoto kwa wazazi kutokuwa sababu za ajali na matukio ya aibu katika maisha ya watoto wao. Mumbi ameandika vitabu viwili kufikia sasa.

Chanzo: BBC