Wananchi zaidi ya milioni 3 wa Sierra Leone waliotimiza masharti ya kupiga kura wameelekea kwenye masanduku ya kupigia kura mapema leo Jumamosi kumchagua rais, wabunge na viongozi wa serikali za mitaa katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.
Rais Julius Maada Bio wa Sierra Leone anagombea muhula wa pili wa urais katika uchaguzi mkuu huo unaofanyika leo, ambapo anawania kupitia chama tawala cha Sierra Leone People’s Party (SLPP).
Bio amejitosa kwenye kinyang'anyiro hicho licha ya makundi ya upinzani kufanya maandamano ya mara kwa mara ya kumtaka aachie madaraka, wakimtuhumu kuwa ameshindwa kuliendesha taifa.
Nchi hiyo yenye jamii ya watu milioni 8.4 hivi sasa inakabiliwa na mfumko wa bei na gharama ya juu ya maisha; changamoto ambazo zimewafanya wapizani wakosoe utendaji kazi wa rais huyo mwenye umri wa miaka 59.
Uchaguzi Sierra Leone Rais Bio anachuana na Samura Kamara (72) ambaye alikuwa pia mgombea wa urais kwa tiketi ya chama cha upinzani cha All People's Congress (APC) katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2018 nchini humo.
Kamara ambaye amewahi kuwa Waziri wa Fedha na Mambo ya Nje wa nchi hiyo, alishindwa na Bio katika duru ya pili ya uchaguzi huo. Mbali na wawili hao, kuna wagombea wengine 11 wanaowania urais katika uchaguzi wa leo.
Mshindi wa urais sharti apate zaidi ya asilimia 55 ya kura, vinginenevyo uchaguzi huo utaingia katika duru ya pili ndani ya wiki mbili zijazo. Bunge la nchi hiyo lina viti 146, ambapo 14 vimetengwa kwa ajili ya viongozi wa kikabila.