Sierra Leone imetengua amri ya nchi nzima ya kutotoka nje usiku iliyotangazwa jana Jumapili huku hali ya utulivu ikirejea, siku moja baada ya watu wasiojulikana na waliokuwa wamejizatiti kwa silaha kushambulia kambi moja ya kijeshi katika mji mkuu wa nchi hiyo Freetown.
Wizara ya Habari ya nchi hiyo imesema ingawaje agizo hilo la kutotoka nje usiku limefutwa, lakini imewashauri wananchi wa nchi hiyo ya Afrika Magharibi kusalia majumbani mwao.
Rais wa Sierra Leone Julius Maada Bio pia ametoa hakikisho kwamba utulivu umerejeshwa katika mji mkuu wa Freetown. Amesema aghalabu ya waliofanya ghasia hizo za jana Jumapili wametiwa mbaroni.
Ingawaje serikali ya Freetown haijatoa maelezo ya kina kuhusu matukio ya jana au kueleza iwapo lilikuwa jaribio la mapinduzi, lakini video zilizosambaa mitandaoni zimewaonyesha wanajeshi waliobeba silaha nzito wakipiga nara wakisema 'tunataka kusafisha Sierra Leone.'
Baadhi ya mashuhuda awali walizieleza duru za habari kwamba, walisikia milio ya risasi na milipuko katika wilaya ya Wilberforce mjini Freetown, kunakopatikana ghala la silaha pamoja na balozi kadhaa za kigeni. Rais wa Sierra Leone Julius Maada Bio
Wakati huo huo, Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi ECOWAS imelaani jaribio la baadhi ya watu la kuchukua silaha na kuvuruga utaratibu wa kikatiba nchini Sierra Leone.
Hali ya kisiasa katika taifa hilo la Afrika Magharibi imesalia kuwa ya wasiwasi tangu kuchaguliwa tena kwa Rais Julius Maada Bio katika uchaguzi uliopingwa na mgombea mkuu wa upinzani mnamo mwezi Juni.
Ghasia za Sierra Leone zimejiri baada ya wimbi la mapinduzi ya kijeshi kushuhudiwa katika eneo hilo la Afrika Magharibi. Mapinduzi 8 ya kijeshi yameshuhudiwa katika maeneo ya Afrika Magharibi na Kati tokea mwaka 2020, yakiwemo mapinduzi ya Mali, Burkina Faso, Niger na Guinea.