Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Siasa ya Mkapa iliiwezesha Rwanda kujiunga EAC

E2ba4f8df2938184d1d7908fbed79ae0 Siasa ya Mkapa iliiwezesha Rwanda kujiunga EAC

Tue, 28 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

RWANDA imesema ina inayafurahia maisha ya Rais wa Awamu ya Tatu wa Tanzania, Hayati Benjamin Mkapa kutokana na siasa yake kuiwezesha kukubaliwa kujiunga Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) mwaka 2007.

Balozi wa Rwanda nchini Tanzania, Charles Karamba alisema hayo ofisini kwake Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na mwandishi wa gazeti la HabariLeo Afrika Mashariki, juzi.

Alisema pamoja na vikwazo vilivyoikabili Rwanda wakati wa kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mkapa hakuchoka kusimama na taifa hilo lililokatika ukanda wa Maziwa Makuu katika kuisaidia kukubaliwa ombi lake.

Alisema Rwanda imejifunza mengi kutokana na maisha ya Mkapa kisiasa kwa sababu siasa yake ilikuwa nzuri na ya kimataifa.

“Alikuwa na siasa ya kuunganisha watu kama alivyotuunganisha sisi, siasa ya kuwafanya maadui wawe marafiki. Tumejifunza mengi kutoka kwake,” aliongeza.

Balozi Karamba alisema ingawa Rwanda ilikubaliwa kujiunga na EAC mwaka 2006 na kusaini rasmi mwaka 2007, juhudi na mipango ya kujiunga na jumuiya hiyo iliyo imara kuliko zote Afrika zilianza wakati Mkapa akiwa Rais.

“Asingekuwa Mkapa huenda leo Rwanda isingekuwa mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Tulimtegemea yeye kutusemea katika vikao vya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki,” alisema Balozi Karamba.

”Rwanda ilikubaliwa kuingia Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 2006 lakini juhudi za kutaka kujiunga na jumuiya hiyo zilianza miaka mitano nyuma, kipindi cha pili cha utawala wa Mkapa,” alisema.

Alisema Wanyarwanda hawawezi kusahau mchango mkubwa wa Rais Mkapa kuwasaidia kuingia katika jumuiya kwa sababu mchango wake ulikuwa mkubwa kwani aliisaidia Rwanda kisiasa kutoka mwanzo hadi tunaingia EAC.

Kwa mujibu wa Balozi Karamba, Hayati Mkapa alikuwa mwanadiplomasia mzuri Afrika hivyo EAC imepoteza nguli wa diplomasia duniani.

Asema juhudi za Mkapa kuisaidia Rwanda kujiunga na Afrika Mashariki zilitanguliwa na juhudi za kuhakikisha Rwanda inakuwa moja na yenye amani kigezo kinachohitajika kufaulu kukubaliwa kwa nchi kujiunga na jumuiya hiyo.

Baada ya Rwanda kuwa na amani, Rais Mkapa alianza kuisaidia nchi jirani ya Burundi kuwa na amani. Balozi Karamba alisema mafanikio ya juhudi zake hizo ya kuleta amani Rwanda na Burundi yalisababisha nchi hizo kukubaliwa kujiunga na EAC kwa pamoja mwaka 2007.

“Faida za Rwanda kujiunga na EAC ni kuwa soko limekuwa kubwa na huru kiasi wananchi wa Rwanda wanaweza kuuza bidhaa zao katika nchi yoyote Afrika Mashariki bila bughudha,” alisema.

Chanzo: habarileo.co.tz