BAADA ya kulegezwa baadhi ya hatua za kudhibiti ugonjwa wa COVID-19 zilizotangazwa tangu mwezi Machi, maisha ya kawaida yameanza kurejea nchini Uganda ambapo maduka makubwa, saluni na usafiri vimeanza kufanya kazi.
Baada ya kipindi cha miezi minne cha kufungwa kwa biashara nyingi katika kitovu cha mji wa Kampala, Rais Yoweri Museveni amelegeza kanuni hizo kwa kile alichokitaja kuwa ni ushauri wa wanasayansi.
Majengo 110 ya maduka yameruhusiwa kufunguliwa lakini kwa masharti makali ya kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wanaepusha maambukizi ya virusi vya corona.
Miongoni mwa masharti hayo ni kuhakikisha kuwa mteja ana barakoa, anapimwa kiwango chake cha joto na pia jina na anwani yake kusajiliwa. Museveni pia amefupisha muda wa kutotoka nje kwa saa mbili.
Tangazo la kulegeza kanuni lilisubiriwa kwa shauku kubwa hususan na waendesha pikipiki za abiria maarufu kama bodaboda wakitarajia kuwa wataruhusiwa kubeba abiria.
Huku akielezea kuwahurumia zaidi ya walimu laki tatu na nusu wa shule na taasisi binafsi za elimu ambao waajiri wao walisitisha kuwalipa mishahara tangu mwezi Machi, kiongozi huyo alifafanua kuwa bado wana mjadala mzito kuhusu suala la kufungua tena shule na taasisi za elimu. Walimu, wazazi na wanafunzi watasubiri kwa mwezi mmoja zaidi kufahamu kama masomo yataanza tena.