Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shirika la Ndege Kenya lashindwa kulipa deni Sh1.9 trilioni

FC7EAA98 6627 4F9E 8532 9C04867F234A.jpeg Shirika la Ndege Kenya lashindwa kulipa deni Sh1.9 trilioni

Sat, 29 Oct 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati Shirika la Ndege la Kenya likiendelea kujiimarisha kwenye uwekezaji na kuongeza idadi ya ndege, taarifa kutoka Ofisi ya Hazina ya Taifa hilo imesema shirika hilo lilishindwa kulipa mkopo wa Sh1.9 trilioni kutoka benki ya Exim Marekani.

Ripoti ya Usimamizi wa Madeni ya Mwaka (mwaka wa fedha wa 2021/2022), imesema licha ya shirika kupewa dhamana yaSh1.2 trilioni kati ya Sh1.9 trilioni za mkopo kutoka Serikalini bado ilishindwa kuurejesha mkopo huo.

Taarifa hiyo pia inaeleza kuwa KQ ilichukua mkopo huo kwa ajili ya kununua ndege mpya saba na injini moja. Hata hivyo taarifa hiyo imesema Serikali imeanza utaratibu wa kulilipa deni hilo

"Serikali ipo katika mchakato wa kulipa deni litakalokamilika katika mwaka wa fedha wa 2022/2023." sehemu ya taarifa hiyo ilisema.

Mtendaji Mkuu wa KQ, Allan Kilavuka alipoulizwa kuhusu kuwepo kwa deni hilo, alisema kiasi cha fedha kilichonukuliwa na Hazina kuwa sio sahihi.

“Thamani inayonukuu ya deni tunalodaiwa na Exim si sahihi; Sh1.1 trilioni ndio deni halali. Sijui kuhusu hizo nyingine… labda wamejumuisha dhamana nyingine,”alisema.

Mkurugenzi wa Hazina ya Kitaifa anayesimamia usimamizi wa madeni, Dk Haron Sirma alisema sababu kubwa iliyofanya deni hilo kushindwa kulipwa ni pamoja na athari za Uviko-19.

"Hatua za kuzuia janga la Uviko-19 ziliathiri vibaya biashara ya ndege ulimwenguni kote ikiwa ni pamoja na KQ. Serikali iliingilia kati deni hili ili kufanya usaidizi wa kifedha ikiwemo kuhakikisha deni hilo linalipwa,”alisema.

Aidha, Kilavuka alisema kutokana Uviko-19 Shirika lililazimika kupunguza baadhi ya shughuli zake hivyo hata mazungumzo ya kulipa deni hilo yalisimama.

"Shirika la ndege (KQ) bado halijaanza kufanya kazi kikamilifu na tumeiomba Serikali kushirikiana nasi kwenye mkopo huu ili kuhakikisha deni hili tunalilipa,”alisema.

Kwa upande wao hazina imesema inafuatilia kwa karibu madeni kutoka kwenye mashirika ya serikali kwasababu yanaleta hatari kubwa za kifedha kwa uchumi.

KQ inamilikiwa na serikali kwa asilimia 48.9 na kundi la benki 10 za Kenya ambazo zinamiliki asilimia 38.1 ya hisa.

Wanahisa wengine ni pamoja na KLM Royal Dutch Airline (asilimia 7.8), wafanyakazi (asilimia 2.4) na wanahisa wengine kwa asilimia 2.8.

Takwimu za shirika la hilo zinaonyesha idadi ya ndege zinazomilikiwa na shirika hilo zimepungua ndani ya miezi tisa iliyopita kutoka 43 hadi 41 mnamo Desemba 31 2021 baada ya ndege mbili za kukodi (Embraer 190) kurejeshwa kwa mkodishaji kufuatia kumalizika kwa mkataba.

Kati ya ndege hizo 41, 18 zinamilikiwa na shirika lenyewe huku 23 zikiwa kwenye mpangilio wa kukodisha. Idadi ya ndege za shirika hilo ilishuka hadi 39 katika mwaka wa 2017 kutoka 52 mwaka 2015, kabla ya kupanda hadi 43 mwaka 2021.

Katika kuhakikisha shirika hilo linajiweka imara kwenye uchumi kwa sasa limeanza upya mijadala ya kukodisha ndege kama hatua za kubana matumizi yake.

Hatua zingine ni pamoja na ushirikishwaji na wanahisa wakuu (serikali) kwa usaidizi wa kifedha, kusitishwa matumizi yasiyo ya muhimu na utekelezaji wa kupunguza kwa mishahara ya muda kwa wafanyakazi.

KQ pia imejipanga kuongeza umakini katika biashara ya mizigo na tayari imebadilisha ndege mbili za abiria kuwa za kubeba mizigo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live