Thamani ya Shilingi ya Kenya, imeendelea kushuka dhidi ya dola ya Marekani na kufikia kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa katika historia yake, inaripoti Gazeti la Business Daily.
Walioathirika zaidi na kuporomoka kwa shilingi hiyo ni watumiaji wake ambao wanalipia gharama kubwa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje.
Kwa mujibu wa gazeti hilo Benki kadhaa za biashara zinauza dola za Kimarekani zaidi ya Sh150 jijini Nairobi, zikizidisha shinikizo kwa shilingi ya Kenya huku zikiweka wateja wake ongezeko jipya la bei inayotokana na sarafu katika bidhaa zinazoagizwa kutoka nje zikiwemo mbolea, vifaa vya elektroniki na magari.
Wastani wa bei ya dola katika benki kadhaa jijini Nairobi na mashirika matatu ya biashara ya kubadilisha fedha yaliyotolewa na gazeti la Business Daily ilikuwa inaelekea Sh150.
Benki Kuu ya Kenya (CBK), hata hivyo, iliweka wastani wa kiwango cha ubadilishaji kuwa Sh142.98, ikionyesha tofauti kubwa kati ya kiwango rasmi na biashara halisi kama ilivyonukuliwa na wafanyabiashara wa fedha.