Ombi la mahakama la kupinga sheria mpya iliyotiwa saini dhidi ya wapenzi wa jinsia moja nchini Uganda limewasilishwa.
Bunge la Uganda lilitangaza kuwa rais Yoweri Museveni ametia saini mswada huo kuwa sheria siku ya Jumatatu.
Ilipitishwa kwa mara ya kwanza mnamo Machi lakini ulirudishwa bungeni kufanyiwa marekebisho.
Ombi hilo linasema kuwa sheria hiyo ni kinyume na inapinga haki ya kutobaguliwa, kwa kuharamisha mahusiano ya watu wa jinsia moja.
Sheria hiyo mpya inataja kifungo cha maisha kwa wale wanaopatikana na hatia ya kufanya mapenzi ya jinsia moja.
Walalamishi hao kutoka Jukwaa la Uhamasishaji na Ukuzaji wa Haki za Binadamu wanaongeza kuwa sheria hiyo ilipitishwa bila kuwapa nafasi walio wachache kutoa maoni yao wakati ilipokuwa ikipitiwa na kamati ya sheria ya bunge.
Sheria hiyo imeshtumiwa pakubwa, na taarifa kutoka kwa wafadhili wakuu wa huduma za afya ikiwa ni pamoja na UN AIDS, ikisema kuwa kuna uwezekano wa kufanya iwe vigumu kwa watu walio katika na mahusiano ya jinsia moja kupata huduma za afya zinazookoa maisha.
Awali, mswada huo ulikuwa umeharamisha kuwatambua walio wachache kijinsia, lakini hii ilirekebishwa baada ya Rais Museveni kudai kuwa ingesababisha kukamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa watu kutokana na muonekano wao.
Sheria sawa na hiyo dhidi ya wapenzi wa jinsia moja ilitupiliwa mbali na mahakama ya kikatiba ya Uganda mwaka 2014, kwa kupitishwa bila akidi inayotakiwa bungeni.