Shirikisho la Kimataifa la Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu, IFRC, limesema Jumanne kwamba shehena ya misaada ya kibinadamu iliyohitajika sana lilifika katika mji wa Port Sudan, huku mapigano zaidi yakiripotiwa kati ya jeshi la Sudan na kundi pinzani la wanamgambo wa RSF.
Misaada hiyo ilijumuisha blanketi, vifaa vya jikoni na vyandarua, kwa familia 500, IFRC ilisema katika taarifa.
Shehena nyingine inatarajiwa katika siku zijazo ikiwa na vifaa vya matibabu.
"Nyingi za vifaa vyetu vya misaada tayari viligawiwa watu wanaohitaji, licha ya baadhi kuporwa huko Khartoum na Darfur," alisema Mkurugenzi wa IFRC wa Kanda ya Afrika Mohammed Mukhier.
"Kwa hivyo, msaada huu wa kimataifa wa kibinadamu, unakuja wakati muhimu kwani utaliwezesha shirika la Hilali Nyekundu la Sudan kusaidia watu waliopatikana kati ya vita na mafuriko yanayofuata, ambayo ni ya kawaida nchini humo."
Tangu mapigano yazuke zaidi ya mwezi mmoja uliopita, takriban watu 600 wameuawa, kulingana na Shirika la Afya Duniani.
Mzozo huo umewakosesha makazi zaidi ya watu 700,000 ndani ya Sudan, huku wengine 200,000 wakikimbilia nchi jirani, Umoja wa Mataifa ulisema.
Jeshi la Sudan, linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, linapambana na Vikosi vya wanamgambo, vinavyoongozwa na Jenerali Mohammed Hamdan Dagalo.
Majenerali hao wawili ni washirika wa zamani ambao kwa pamoja walipanga mapinduzi ya kijeshi ya Oktoba 2021, ambayo yalivuruga mchakato wa mpito kwa utawala wa kiraia, kufuatia kuondolewa madarakani kwa kiongozi wa muda mrefu Omar al-Bashir mnamo mwaka wa 2019.