Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yaonya kuhusu usalama wa nyama za kuku

Kuku Nyama (18).jpeg Serikali yaonya kuhusu usalama wa nyama za kuku

Mon, 13 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali ya Kenya imetoa tahadhari kuhusu usalama wa nyama ya kuku inayouzwa Nairobi na miji mingine mikuu nchini.

Kwenye barua, mkurugenzi wa Idara ya Afya ya Mifugo Obadia Njagi alisema nyama nyingi zinazouzwa katika maduka mengi hazijakaguliwa na maafisa wa afya.

Kulingana na Bw Njagi, nyakati hizi kuku huchinjwa katika maboma ya watu badala ya vichinjio maalum inavyohitajika kisheria.

Aliongeza kuwa usafirishaji nyama inayotolewa kutoka maboma ya watu binafsi na kupelekwa kwenye maduka unakiuka kanuni zilizowekwa za usalama na usafi.

“Nyama hii hupatikana moja kwa moja kutoka kwa wafugaji wa kuku wa nyama, ambao huwachinja katika vibanda vyao na kuisafirisha hadi kwa mikahawa na vioski vya kuuza chakula. Nyama hii sio salama,” Njagi akaonya kwenye barua hiyo iliyonakiliwa kwa makurugenzi wa Idara hiyo katika ngazi za kaunti.

Maduka yaliyolengwa zaidi ni yale yanayouza vyakula vya kisasa (fast food) katikati mwa jiji la Nairobi na miji mingine nchini.

Vichinjio vingi nchini vinalaumiwa kwa kutoa nyama ya kuku moja kwa moja kutoka kwa wafugaji kuku.

“Hii ni kinyume na Sheria ya Kusimamia Usalama wa Nyama, Kifungu cha 356 inayosema kuwa wanyama wa kuliwa sharti wachinjwe katika vichinjio vilivyoidhinishwa na kupewa leseni na ambavyo hukaguliwa na maafisa husika,” akasema.

Bw Njagi aliwashauri wakaguzi wa nyama katika kaunti kufuatilia kwa makini mwenendo huo mbaya unaoweka maisha ya Wakenya hatarini.

Idara hiyo pia imeonya kuwa wafanyabiashara watakaopatikana na hatia ya kukiuka sheria na mahitaji kuhusu nyama ya kuku watachukuliwa hatua kali.

“Maovu kama hayo huwaweka wateja katika hatari ya kununua nyama isiyo salama na yenye vimelea vya kusababisha maradhi,” barua hiyo ikasema.

Biashara za kuchinja na kuuza nyama za kuku zinazidi kunoga mitaa mingi Nairobi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live