Serikali ya Sudan Jumatatu ilikataa kushiriki katika mkutano wa kikanda wenye lengo la kumaliza miezi mitatu ya mapigano ya kikatili, ikiishtumu Kenya ambayo inasimamia mazungumzo hayo, kukipendelea kikosi hasimu cha wapiganaji.
Mapambano ya madaraka kati ya mkuu wa jeshi la Sudan Abdel Fattah al-Burhan na makamu wake wa zamani Mohamed Hamdan Dagalo, kamanda wa kikosi cha dharura (RSF), yaligeuka vita katikati ya mwezi Aprili na tangu wakati huo, yameua maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuhama makazi yao.
Jumuia ya nchi za Afrika Mashariki (IGAD) jana Jumatatu iliwaalika mahasimu hao kwenye mkutano katika mji mkuu wa Ethiopia, huku mapigano yakizidi kupamba moto kote nchini Sudan.
Si Burhan wala Dagalo hakuna aliyehudhuria mazungumzo hayo mjini Addis Ababa, ingawa kikosi cha RSF kilituma mwakilishi wake kwenye mkutano wa nchi nne uliongozwa na Kenya, Sudan Kusini, Djibouti na Ethiopia.
Tangu Aprili 15, takriban watu 3,000 wameuawa katika machafuko hayo, kulingana na shirika lisilo la kiserikali linalofuatilia migogoro (ACLED), lakini idadi ya vifo inaaminika kuwa kubwa zaidi kwani bado ni vigumu kufika kwenye maeneo mengi ya nchi.