Maafisa wa serikali ya Nigeria wamesema wana wasiwasi baada ya mamia ya watu kuingia mitaani katika jimbo la kati la Niger na jimbo la kaskazini magharibi la Kano siku ya Jumatatu ilikulalamika kutokana na kuendelea kupanda kwa bei za chakula na ughali wa maisha.
Waziri wa fedha Olawale Edun, akizungumza Abuja siku ya Jumatatu wakati wa mkutano na ujumbe kutoka Ujerumani, amesema, serikali ina wasiwasi kuhusu ongezeko la bei na inalishighulikia tatizo hilo.
Alilaumu kwamba ongezeko la hivi karibuni la bei za chakula linatokana na kuongezeka mahitaji, akisema njia pekee ya kusuluhisha hali hii ni kuimarisha uzalishaji wa kilimo
Maafisa wa polisi katika mji mkuu wa jimbo la Niger wa Minna, wamesema waliwatawanya waandamanaji kwa kutumia “nguvu kidogo” lakini waandamanaji wametishia kurudi.
Kwa miezi, Wanigeria wamekuwa wakilalamika kutokana na hali ya uchumi wa nchi hiyo ambao umebaki kusuasua wakati wa mageuzi ya sera za serikali.
Mwezi mei mwaka jana Rais Bola Tinubu alichukua hatua ya kijasiri na kutangaza mageuzi ya kiuchumi, ikiwa ni pamoja na kuondoa ruzuku za mafuta na aliacha thamani ya sarafu ya taifa, naira kufuata muelekeo wa masoko huru.