Jana Jumatano serikali ya Libya ilianzisha operesheni ya kuwafukuza na kuwarejesha makwao wahamiaji haramu 270 waliozuiliwa nchini humo wakati walipokuwa wanajaribu kuelekea barani Ulaya.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Libya, Emad al-Tarabelsi amesema hayo na kuongeza kuwa, ndege kadhaa zitatumika kuwasafirisha wahamiaji hao kutoka Tripoli hadi kwenye nchi zao za asili ambazo ni Somalia, Sudan, Nigeria na Bangladesh.
Aidha waziri huyo wa Libya ameahidi kupambana na uhamiaji haramu na magendo ya binadamu nchini humo, akilalalamika kwamba biashara hiyo haramu inawaweka wahamiaji hao katika hatari nyingi zikiwemo za kufa maji baharini.
Ameongeza kuwa, Libya ambayo imegeuka kuwa kitovu cha wahamiaji inapata hasara kubwa ya "kuwahifadhi na kuwasaidia" wahamiaji haramu kila pale wanapokamatwa na kuzuiliwa kwenye vituo vya serikali. Kila leo maiti za wahamiaji haramu zinaokotwa kwenye fukwe za Libya
Wahamiaji haramu, wengi wao wakiwa wa nchi za Afrika za kusini mwa Jangwa la Sahara, wanatumia fursa ya ukosefu wa usalama na machafuko nchini Libya tangu 2011 kujaribu kuvuka Bahari ya Mediterania kuelekea pwani za nchi za Ulaya. Lakini wengi wa wahamiaji hao wanaishia kufa maji baharini kutokana na kutumia mitumbwi dhaifu ya plastiki ambayo haihimili mawimbi makali ya Bahari ya Mediterania. Wahamiaji wengi huishia mikononi mwa magenge ya magendo ya wanadamu na kupigwa mnada masokoni kama bidhaa.
Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji, tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 2023 hadi hivi sasa, wahamiaji haramu 10,646 wameokolewa na kuhifadhiwa na serikali ya Libya.
Mwishoni mwa mwezi Julai mwaka huu, Waziri Mkuu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya, Abdul Hamid al-Dbeibeh aliisema kuwa, jumuiya ya kimataifa inapaswa kutoa msaada wa kisiasa, kimaada na kiusalama kwa Libya katika suala zima la kukabiliana na wahajiri haramu.Al-Dbeibeh alitoa wito wa kuweko ushirikiano wenye uwiano na Umoja wa Ulaya katika suala la wahajiri na kuongeza kuwa: Libya haina ni yoyote ya kuwapa makazi wahajiri haramu katika nchi zinazotumiwa na wahajiri hao kama njiia ya kuelekea Ulaya.