Serikali ya Kenya imewatambua rasmi watu wa jamii ya Pemba, ambao hawakuwa na uraia wa nchi yoyote kama kabila la Kenya.
Kupitia taarifa rasmi ya serikali, Rais William Ruto amesema kuwa uamuzi huo umefikiwa baada ya kuangalia hoja zilizowasilishwa na kamati mbali mbali za bunge kwa ajili ya kutambuliwa kwa jamii hiyo.
Kutambuliwa kwa Wapemba kutawawezesha watu wa jamii hiyo kuingizwa katika makabila mengine ya kupata huduma muhimu kama vile elimu, huduma ya afya, maslahi ya kijamii, huduma za kifedha, na ajira.
Watu wa jamii ya Pemba zaidi ya 8,000 ambao wameishi katika kaunti za pwani ya Kenya za Kwale, Kilifi, Mombasa na Lamu wameishi bila utaifa kwa miongo kadhaa.
Wengi wao wamekuwa wakijishugulisha na uvuvi wa mbali baharini na kilimo kama shughuli zao kuu za kiuchumi.
Wamekuwa wakilalamikia kuhusu kukamatwa na polisi wa Kenyana walinzi wa mwambao kwa kukosa nyaraka za utambulisho.
Uamuzi huo umepokelewa na Shirika la Umoja wa Maraifa la Wakimbizi na makundi ya haki za binadamu ambayo yamekuwa yakishinikiza kutambuliwa kwa Wapemba.
Watu wa jamii hiyo wanadai ni vizazi vya wahamiaji kutoka Zanzibar waliokuja wakati wa utawala wa Sultan Bin Khalifa katika miaka ya 1800.
Katika miaka ya hivi karibuni serikali ya Kenya iliyatambua makabila mengine ya watu ambao hawakuwa na uraia wa nchi yoyote ile wakiwemo Wamakonde, Washona, na jamii ya watu wa Asia Kusini.