Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali ya Kenya yaahirisha kufunguliwa kwa shule kutokana na mvua kubwa

Serikali Ya Kenya Yaahirisha Kufunguliwa Kwa Shule Kutokana Na Mvua Kubwa Serikali ya Kenya yaahirisha kufunguliwa kwa shule kutokana na mvua kubwa

Mon, 29 Apr 2024 Chanzo: Bbc

Serikali imeahirisha kufunguliwa kwa shule hii leo hadi Jumatatu, Mei 6, 2024.

Katika taarifa yake, Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu alisema wamepokea data kwamba baadhi ya shule zimeathiriwa vibaya na mafuriko yanayoendelea.

Alisema kuwapeleka wanafunzi na wafanyikazi katika shule zilizoathiriwa itayaweka maisha yao hatarini, hatua iliosababisha kuahirishwa kufunguliwa tena.

"Athari mbaya za mvua katika baadhi ya shule ni kubwa sana hivi kwamba halitakuwa jambo la busara kuhatarisha maisha ya wanafunzi na wafanyikazi kabla ya hatua za kuzuia maji kuchukuliwa ili kuhakikisha usalama wa kutosha wa jamii zote za shule zilizoathiriwa.

“Kutokana na tathmini hii, Wizara ya Elimu imeazimia kuahirisha kufunguliwa kwa shule zote za msingi na sekondari kwa wiki moja hadi Jumatatu, Mei 6, 2024,” Machogu alisema.

Shule zilipangwa kufunguliwa tena Aprili 29 (Leo).

Waziri alisema Wizara yake itashirikiana na mashirika na wadau husika kuweka mikakati ya kukabiliana na athari za mvua.Aliongeza kuwa pia watatoa taarifa za mara kwa mara kuhusu hatua zote zilizopigwa kuhusu sekta ya elimu.

Siku ya Jumapili, Jumuiya ya Kitaifa ya Wazazi ilipendekeza mabadiliko ya tarehe za kufunguliwa kwa shule katika maeneo yaliyoathiriwa.

Haya yanajiri huku idara ya utabiri wa hali ya anga ikionya kuhusu mvua kubwa zaidi katika siku zijazo huku zaidi ya watu 90 wakiripotiwa kufariki na wengine wengi kujeruhiwa au kutoweka.

Chanzo: Bbc