Serikali ya Kenya sasa itaanza kusikiliza mazugumzo ya simu baada ya kuruhusiwa na Mahakama ya Juu huku wadau wa masuala ya haki za binadamu wakisema kuwa uamuzi huo utavuruga uhuru wa kulinda na kuhifadhi siri ya mazugumzo ya wananchi.
Ikitupilia mbali rufaa iliyowasilishwa na Chama cha Wanasheria Kenya (LSK) mahakama hii ya upeo ilisema ipo haja ya kupiga teke vifaa duni vya mawasiliano.
Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu na Majaji wa mahakama ya juu Mohammed Ibrahim, Smokin Wanjala, Njoki Ndung’u na Isaac Lenaola walikubaliana na uamuzi wa Mahakama ya Rufaa kwamba CAK yapasa kuendelea kustawisha kifaa cha kuboresha unasaji wa mawasiliano kuhakikisha usalama upo kwa wote.
Majaji waliotoa uamuzi huo katika mahakama ya rufaa ni Jaji Mkuu Martha Koome, Jaji William Ouko na Jaji Daniel Musinga.
Jaji Koome, Ouko na Musinga walibatilisha ujamuzi wa Jaji John Mativo aliyefutilia mbali uamuzi wa CAK kutaka kampuni za mawasiliano Safaricom, Airtel, na Orange Telkom Kenya kuweka kifaa maalum katika mitambo yake kusikiza mazugumzo ya simu ya kila mtu.
Jaji Mativo alikubaliana na Seneta wa Busia Okiya Omtatah kwamba itakuwa ni ukiukaji wa haki za usiri wa mawasiliano mtu mwingine kusikiza mazugumzo baina ya wananchi.
CAK ilikata rufaa kupinga uamuzi wa Jaji Mativo kuhifadhi usiri wa mawasiliano baina ya wananchi kwa njia ya simu.
Bw Omtatah alilalama katika mahakama kuu kwamba kuruhusu CAK kuweka mtambo maalum wa mawasiliano almaarufu DMS (devise management system) ni ukiukaji wa siri ya kuhifadhi mazugumzo baina ya Wakenya.
Ikijitetea CAK ilisema kuwekwa kwa kifaa hiki DMS katika mitambo ya kampuni za mawasiliano ililenga kutambua simu duni.
Jaji Mativo alizuia CAK kuweka mtambo wa DMS ili kunasa mawasiliano katika simu zote na kutambua mawasiliano katika mitambo ya IMEI, IMSI, MISSDN na CDRs ya wamiliki wa simu.
Majaji Koome, Ouko na Musinga walibatilisha uamuzi huu na kuruhusu CAK kuboresha na kustawisha mtambo huu wa DMS.
LSK ilikata rufaa kupinga uamuzi wa Jaji Koome, Ouko na Musinga na kusema haki za wamiliki wa simu na uhuru wa mawasiliano miongoni mwa wananchi.
CAK ilipinga rufaa hiyo ikisema LSK haikushiriki katika kesi hiyo ya Omtatah katika Mahakama Kuu na pia katika Mahakama ya Rufaa.
Majaji Mwilu, Ibrahim, Wanjala, Ndung’u na Lenaola walisema LSK haina mamlaka kuwasilisha rufaa hiyo kupinga kuwekwa kwa kifaa cha DMS katika mitambo ya mawasiliano.
Mahakama ya Juu ilisema rufaa ya LSK imepotoka na kamwe haitaruhusu watu wasioridhika na maamuzi ya korti kuwasilisha rufaa kiholela.