Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Senegal kutangaza tarehe mpya ya uchaguzi

Rais Wa Senegal Aahirisha Uchaguzi Senegal kutangaza tarehe mpya ya uchaguzi

Sun, 18 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali ya Senegal imetangaza kuwa, uchaguzi wa rais ulioahirishwa utafanyika haraka iwezekanavyo.

Tangazo hilo la serikali linakuja siku moja tu baada ya Baraza la Katiba la nchi hiyo kubatilisha amri ya rais Macky Sall ya kuusogeza mbele kwa miezi kadhaa uchaguzi wa nchi hiyo.

Msemaji wa Rais Sally, Yoro Dia amesema kuwa rais anakusudia kuheshimu maamuzi hayo ya Baraza la Katiba ambalo limesema kuwa kuuchelewesha uchaguzi huo uliopangwa mnamo Februari 25 hadi Desemba 15, ni kinyume na katiba. Hata hivyo msemaji huyo hakutaja tarehe mpya ya uchaguzi.

Kulingana na hukumu iliyopitishwa na wajumbe wake saba, Baraza la Katiba la Senegal lilifuta amri iliyotiwa saini na Rais Sall, ambayo iliakhirisha uchaguzi wa rais uliokuwa umepangwa kufanyika Februari 25.

Ghasia ziliibuka Senegal baada ya Rais Macky Sall kutoa tangazo la kuakhirisha uchaguzi hadi Disemba mwaka huu (2024)

Wagombea urais wa upinzani na wabunge walikuwa wamewasilisha changamoto kadhaa za kisheria kwa mswada uliopitishwa na bunge wiki iliyopita, ambao pia ulirefusha muda wa Rais Macky Sall kubaki madarakani katika kile ambacho wakosoaji wanasema ni sawa na "mapinduzi ya kitaasisi."

Tangazo la kuahirishwa uchaguzi huo, ambalo lilitolewa wiki chache tu kabla ya upigaji kura, lilizua makabiliano makali kati ya waandamanaji na askari wa usalama katika mji mkuu Dakar na maeneo mengine ya mijini.

Watu watatu waliuawa katika maandamano ya upinzani nchini Senegal yaliyofanywa kulalamikia kuakhirishwa kwa uchaguzi, huku wasiwasi ukiongezeka wa kufutika demokrasia katika moja ya nchi zilizosalia katika eneo la Afrika Magharibi lililokumbwa na wimbi la mapinduzi ya kijeshi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live