Mwenyekiti wa sasa wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS, rais wa Nigeria Bola Tinubu ameamua kuahirisha ziara yake katika mji mkuu wa Senegal, Dakar. Mwenyekiti wa ECOWAS akiwa pia rais wa Nigeria alitakiwa kukutana na Rais Macky Sall nchini Senegal, wakati hali ikiendelea kuwa tete nchini humo baada ya kutangazwa kuahirishwa kwa uchaguzi wa urais.
Ziara ya mkuu wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS) na Rais wa Nigeria, Bola Tinubu, iliyopangwa kufanyika Februari 12, 2024, imeahirishwa bila tarehe mpya kutangazwa, kulingana na chanzo kutoka ikulu ya rais wa Senegal.
Mkuu wa ECOWAS alikuwa akutane na Rais Macky Sall siku ya Jumatatu alasiri, huku hali ikiwa bado ya wasiwasi nchini Senegal, tangu kutangazwa kuahirishwa kwa uchaguzi wa urais kutoka Februari 25 hadi Desemba 15.
Wiki iliyopita, ECOWAS iliitaka Senegal "kurejesha haraka kalenda ya uchaguzi". Na, tangu Ijumaa, vijana watatu wamefariki, waliuawa wakati wa maandamano ya kupinga kuahirishwa kwa uchaguzi wa urais.
Hata hivyo, ujumbe wa waangalizi wa uchaguzi wa Umoja wa Ulaya unatangaza kurejea kwa waangalizi wake 32 wa muda mrefu "kwa kuzingatia kutokuwa na uhakika wa kalenda ya uchaguzi". Ujumbe huo pia unasema kuwa una wasiwasi kuwa uamuzi wa kuahirisha uchaguzi wa urais unaweza kusababisha "kuvunjika kwa utamaduni wa muda mrefu wa demokrasia ya Senegal".