Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sekretarieti EAC yapongeza ushindi wa Rais Magufuli

Ae9b0010cb47bbe880df8f0d17dcf927.png Sekretarieti EAC yapongeza ushindi wa Rais Magufuli

Tue, 10 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

SEKRETARIETI ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imempongeza Rais John Magufuli kwa kuchaguliwa kuongoza Tanzania kwa kipindi cha pili cha miaka mitano na kuvitaka vyama vya siasa vilivyoshiriki uchaguzi huo kuheshimu maamuzi ya wananchi na kukubali matokeo.

Aidha, imewapongeza Watanzania kwa kuwezesha mchakato wa uchaguzi kufanyika kwa amani na kuwa wa demokrasia katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Barua ya pongezi iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa EAC, Balozi Liberat Mfumukeko inaeleza kuwa kwa niaba ya jumuiya hiyo Sekretarieti ya EAC inatoa pongezi kwa Rais Magufuli, serikali na Watanzania kwa kuchaguliwa tena kwa kipindi cha pili kuwa Rais wa Tanzania kwa kura za kishindo katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 28, mwaka huu.

“Jumuiya ina furaha kuwa uchaguzi mkuu ulikuwa na sifa zote za amani, uwazi na demokrasia,” ilisema sehemu ya barua hiyo kwenda kwa Rais Magufuli.

“Pia ni ushahidi wa kuendelea kwa demokrasia na utawala bora kama ilivyoainishwa katika Mkataba wa Kuanzishwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, hivyo tunavisihi vyama vyote vilivyoshiriki uchaguzi kuheshimu matakwa ya Watanzania na matokeo ya uchaguzi.”

“Jumuiya inakutakia mafanikio makubwa zaidi katika kipindi cha miaka mitano ijayo kuhusu mipango yako ya kupambana na rushwa, kukuza maendeleo ya miundombinu, kukuza ukuaji wa uchumi na kukuza utoaji elimu na huduma za afya kwa Watanzania wote pamoja na masuala mengi mazuri,” aliongeza.

Balozi Mfumukeko alisema kulingana na vigezo vya uchaguzi viliyoainishwa katika Mwongozo wa Uchaguzi Katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, uchaguzi huo ulikidhi vigezo vyote na ulikua huru na haki.

Katika uchaguzi huo, Rais Magufuli alishinda kwa kupata kura 12,516,252 sawa na asilimia 84.4 ya kura zote zilizopigwa, huku anayemfuatia akiwa Tundu Lissu kutoka Chadema akipata kura 1,933,271.

Chanzo: habarileo.co.tz