Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa amefanya mazungumzo na wajumbe wa Chama tawala cha African National Congress (ANC), huku shinikizo zikizidi kumtaka ajiuzulu au alazimishwe kutoka ofisini.
Msemaji wa Rais, Vincent Magwenya amewaambia waandishi wa Habari kuwa Ramaphosa anazingatia njia kadhaa na kushauriana na baadhi ya wahusika katika chama tawala ANC.
Hatua hiyo, inajiri kufuatia uchunguzi wa Bunge kubaini kuwa huenda alikiuka sheria za nchi dhidi ya ufisadi kuhusiana na madai ya wizi wa kiasi kikubwa cha fedha katika shamba lake la Phala Phala game.
Sarafu ya Afrika Kusini, randi, ilishuka kwa karibu asilimia tatu mapema wakati Ramaphosa alipoghairi kipindi cha maswali na majibu kilichokuwa kimepangwa bungeni kufuatia kuchapishwa kwa ripoti ya kashfa hiyo.