Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Samatta kuikosa Tunisia

B8fd93384505a478d80ddd9f690450a2 Samatta kuikosa Tunisia

Wed, 11 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

NAHODHA wa Timu ya Soka Taifa, ‘Taifa Stars’ Mbwana Samatta huenda akazikosa mechi mbili dhidi ya Tunisia kutokana na kuwa majeruhi.

Stars inatarajiwa kucheza na Tunisia keshokutwa mjini Tunis kabla ya kurudiana Dar es Salaam baada ya siku tano.

Kwa mujibu wa radio Efm, Samatta aliumia wakati akiitumikia klabu yake ya Fenerbahce ya Uturuki iliyotoka kupoteza mabao 2-0 dhidi ya Konyaspor katika mchezo wa Ligi Kuu mwishoni mwa wiki iliyopita.

Samatta alipohojiwa alisema: “mechi ya mwisho ya ligi nilipata maumivu ya misuli na nilifanyiwa vipimo na majibu yametoka mabaya natakiwa kuwa nje kwa zaidi ya siku 10,”

“Ripoti ya daktari inaeleza napaswa kupumzika ili misuli irejee katika hali ya kawaida, imeniumiza sana lakini sina jinsi nilitamani kuwepo kama kiongozi wa timu lakini sina namna na nimekuja kuongea na vijana na mwalimu nijue hali yao ikoje,”alisema.

Timu wakati wowote itakwenda Tunisia ikitokea Uturuki ilipokwenda kwa maandalizi.

Bado timu ya taifa ina kikosi kipana chenye wachezaji wengi wenye vipaji huenda wale watakaochukua nafasi yake wakatumia fursa ya kufanya vizuri ili kuendelea kuaminiwa.

Hata hivyo, Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Clifford Ndimbo alisema daktari wa Stars ndiye atakayetoa taarifa kamili kuhusu majeruhi wote na kwamba wao bado hawajazipata taarifa hizo.

Katika hatua nyingine, CAF imeruhusu watazamaji kwenye mchezo wa kufuzu Afcon kati ya Tanzania na Tunisia utakaochezwa Novemba 17, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa.

CAF imeelekeza kuwa idadi ya watazamaji watakaoingia kuwa ni asilimia 50 ya uwezo wa uwanja.

TFF inawasiliana na serikali ili kukidhi matakwa ya CAF katika mechi hiyo.

CAf imefanya hivyo kutokana na kujikinga na homa ya corona. Mechi zote zinazochezwa chini ya CAF huwa hazina mashabiki, lakini CAF imeruhusu hilo kwa Tanzania kutokana na kutokuwepo maambukizi ya corona.

Chanzo: habarileo.co.tz