Jumapili ndo kitapigwa kile kipute cha fainali ya Kombe la Ligi huko Wembley.
Mchezo huo utamshuhudia supastaa wa Tanzania, Mbwana Samatta akiwa na majukumu ya kuongoza safu ya ushambuliaji ya Aston Villa kukabiliana na Manchester City ya moto chini ya kocha wake Mhispaniola, Pep Guardiola.
Man City itaingia uwanjani kwenye fainali hiyo ikiwa kwenye makali baada ya kushinda mechi zake tatu zilizopita, West Ham United na Leicester City kwenye Ligi Kuu England na Real Madrid kwenye Ligi Kuu England tena uwanjani Santiago Bernabeu.
Aston Villa wao mambo ni tofauti, wamepoteza kwenye mechi tatu zilizopita, walichapwa na Bournemouth, Tottenham Hotspur na Southampton. Lakini, mchezo wa kesho ni fainali na kila kitu kitaangaliwa kwenye mchezo huo.
Aston Villa watarudi Wembeley kwa mara yao ya tatu katika kipindi cha miaka mitatu, ambapo huko walicheza hapo kwenye mchujo wa kupanda daraja dhidi ya Derby County mwaka jana na dhidi ya Fulham mwaka mmoja kabisa. Kesho wataingia uwanjani kusaka taji lao kubwa ambalo kwa mara ya mwisho kubeba Kombe la Ligi ilikuwa 1996. Wapinzani wao Man City wao wamekuwa wakijibebea tu taji hilo kwa miaka ya karibuni, wakibeba mara tano kwa kuanzia mwaka 2014.
Lakini, fainali hiyo ya kesho itahusu zaidi mambo ya pesa. Michuano ya Kombe la Ligi inaanza kuhesabika pesa baada ya kufika nusu fainali, hivyo Aston Villa, Man City, Man United na Leicester City zote zinakuwa kwenye mgawo.
Kwa ujumla wake zawadi ya pesa ni Pauni 200,000, ambazo zinawawia kuanzia kwenye nusu fainali, ambapo Leicester City na Man United, walipewa Pauni 25,000 kila mmoja.
Aston Villa na Man City kwa kufika fainali, zimejihakikishia shea kubwa kwenye mgawo huo, ambapo atakayefungwa fainali, atalipwa Pauni 50,000 na mshindi ataweka kibindoni Pauni 100,000. Hii itakuwa mechi ya kwanza kwa Samatta kucheza Wembley, akiweka rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza kwenye uwanja huyo wenye hadhi kubwa huko Ulaya.
Kazi ni kwake Samatta kuipa Aston Villa taji na Pauni 100,000 au kukubali kichapo na kuishia tu kuvaa medali za kuwa washindi wa pili na mkwanja wa Pauni 50,000.