Wakenya wamekuwa wakitoa heshima zao kwa Mukami Kimathi, mjane wa mwanaharakati wa kupigania uhuru wa Mau Mau nchini Kenya, Dedan Kimathi.
Familia ya Bi Kimathi iliviambia vyombo vya habari kwamba alipata matatizo ya kupumua Alhamisi usiku na kupelekwa hospitali katika mji mkuu, Nairobi, ambako alifariki muda mfupi baadaye.
Mumewe, ambaye alikuwa kiongozi wa uasi wa Mau Mau, alitekwa, akahukumiwa na kunyongwa na serikali ya kikoloni ya Uingereza mwaka wa 1956.
Alizikwa katika gereza la Kamiti nje kidogo ya jiji. Siku ya Ijumaa, Rais wa Kenya William Ruto alitoa pongezi kwa Bi Kimathi kwa "kustahimili ukatili wa ukandamizaji wa wakoloni, kwa kujivunia makovu ya vita na kubeba hasara mbaya za vita kwa ujasiri wa kustaajabisha".
Naibu Rais Rigathi Gachagua alimtaja kama "mama wa mapambano yetu ya ukombozi na mwanga wa matumaini unaowazunguka wapigania uhuru na vizazi vyao".
Katika maisha yake, alisukuma mijadala kuhusu ustawi wa wapigania uhuru - ambao hawakufurahia manufaa ya kujitolea kwao kwa ajili ya uhuru wa Kenya. Mnamo Januari, alizuiwa kutoka hospitali alikokuwa amelazwa baada ya familia yake kushindwa kulipa gharama- ambayo ilionekana kama dalili ya umaskini ambao wapigania uhuru walipaswa kuvumilia.
Aliruhusiwa baadaye baada ya rais kufuta gharama kiasi cha $7,300 (£5,800). Pia alikuwa akishinikiza kufukuliwa kwa mabaki ya mumewe kutoka gerezani ili kuzikwa upya nyumbani kwake.
Hata hivyo, utafutaji wa miaka mingi wa mahali ambapo alizikwa umeambulia patupu - licha ya Bi Kimathi kueleza nia yake ya kuoneshwa kaburi kabla ya kifo chake.