Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

SADC yampongeza, yamkaribisha Samia

Deb6c9caa0595bf320b6ebab304b0283 SADC yampongeza, yamkaribisha Samia

Thu, 24 Jun 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MWENYEKITI wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Rais Felipe Nyusi wa Msumbiji amemkaribisha Rais Samia Suluhu Hassan katika jumuiya hiyo akiwa Rais.

Rais Samia Juni 23 alikuwa miongoni mwa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC waliohudhuria Mkutano wa Dharura mjini Maputo nchini Msumbiji uliohudhuriwa na marais kadhaa wa nchi hizo, viongozi wengine na wawakilishi.

Rais Samia amehuhudhuria katika mkutano huo kwa mara ya kwanza akiwa Rais wa nchi.

“Nimkaribishe sana Rais Samia katika mkutano huu, amehudhuria kwa mara ya kwanza kama Rais wa Tanzania. SADC inajivunia kupata Rais mwanamke wenye weledi mkubwa sana, tunampongeza,” alisema Rais Nyusi.

Rais Samia alishika hatamu ya kuuongoza Tanzania, Machi 19, mwaka huu alipoapishwa baada ya kifo cha mtangulizi wake, Dk John Magufuli siku mbili nyuma. Kabla ya hapo, alikuwa Makamu wa Rais.

Akifungua mkutano huo, Rais Nyusi alisema hakuna serikali inayoweza kupambana peke yake katika janga la mlipuko wa homa kali ya mafua inayosababishwa na virusi vya corona (Covid-19) bila kusaidiana na wengine.

Hivyo jumuiya hiyo imepitisha maamuzi ya jinsi ya kukabiliana na corona kwa pamoja na kusema ni lazima nchi wanachama wa SADC washirikiane na waelimishe wananchi wao kuchukua hatua dhidi ya janga hilo.

Rais Nyusi alisema janga la corona limeathiri nchi mbalimbali duniani zikiwamo za SADC, na kwamba hakuna budi mapambano dhidi ya maradhi hayo yakafanywa kwa ushirikiano wa serikali na sio kila nchi kupambana kivyake.

“Hakuna serikali inayoweza kupambana peke yake katika janga la corona, lazima tusaidiane na ndiyo maana SADC ilipitisha maamuzi ya jinsi ya kukabiliano na sorona kwa pamoja,” alisema Rais Nyusi.

Awali, Katibu Mtendaji wa SADC, Dk Stegomena Tax alisema wakati huu wa kupambana na corona na tishio la wimbi la tatu la ugonjwa huo, SADC inapaswa kuendelea kuchukua tahadhari.

“Nchi zote wanachama hazijaathiriwa kwa namna sawa, matazamio ya uchumi kwa nchi zetu yatashuka na nchi mbalimbali zimeweka jinsi za kuimarisha uchumi katika kipindi hiki cha mlipuko wa corona,” alisema Dk Tax.

Akifafanua juhudi zilizochukuliwa na viongozi wa SADC kwenye mapambano dhidi ya virusi vya corona, alisema viongozi hao wameendelea kuwa imara wakati huu wa mapambano huku wakijizatiti kutafuta suluhu ya maradhi hayo.

“Natoa shukrani kwa viongozi wetu, wameendelea kubaki imara wakati huu wa mapambano dhidi ya corona, wameendelea kuimarisha utafiti na dawa zikiwemo dawa za asili na juhudi zote za kuleta chanjo zinapokelewa na Sekretarieti inasaidia ukanda wetu,” alifafanua Katibu Mtendaji wa SADC.

Alisema janga la corona limeleta ulazima wa kuchukua hatua za makusudi kukabiliana nao na SADC itaendelea kujifunza kutokana na hali za dharura na kuweka mipango ya maendeleo ya ya jumuiya hiyo.

Akizungumzia masuala ya ugaidi, Mwenyekiti wa SADC alisema bado ni tishio kimataifa na lazima SADC iendelee kupata taarifa muhimu za ugaidi na kuangalia jinsi ya kumaliza tatizo hilo kwenye ukanda wao.

Alisema vitendo vya kigaidi vilivyotokea katika Jimbo la Cabo Delgado Kaskazini mwa Msumbiji vilidhibitiwa na jeshi, lakini akaongeza kuwa na nguvu ya pamoja baina ya nchi za SADC inahitajika kukomesha vitendo hivyo ili visisambae katika nchi za jumuiya hiyo.

Awali Dk Tax pia alizungumzia jambo hilo na kusema hatua mbalimbali zilichukuliwa na SADC kukabiliana nalo, huku mkutano wa hivi karibuni wa TROIKA ukitoa mapendekezo yake ambayo yatawasilishwa hivi karibuni jinsi ya kukomesha vitendo hivyo na vingine vya tishio la usalama na ulinzi.

Aidha, Rais Nyusi alisema nchi za SADC zinakabiliwa na mabadiliko ya hali ya hewa hivyo ni lazima jumuiya hiyo ikajipanga na kujua jinsi ya kukabiliana nayo kwani yameleta athari kwenye ukanda huo.

“Mabadiliko ya hali ya hewa yanaendelea na yana athari kwenye ukanda wetu, ndio maana SADC imeridhia kuanzishwa kwa kituo cha dharura kitakachokuwa kinashughulikia masuala ya majanga na misaada ya kibinadamu kwenye nchi hizo,” alisema Rais Nyusi.

Kuhusu Jukwaa la Biashara la SADC, mwenyekiti huyo alisema litatoa fursa ya kuimarisha na kuhimiza biashara na kusambaza fursa nyingine kwenye utalii, nishati na uwekezaji katika nchi wanachama.

Alisema jukwaa hilo litakuwa na uhusiano wa kikanda na kuwezesha wadau kushirikiana mawazo ya mapendekezo ya maendeleo katika ukanda wa SADC hivyo kukuza uchumi na kuinua hali za wananchi wake.

Alisema masoko yataendelezwa na kuwekewa mpango kazi wa kujenga viwanda vya ndani ya SADC na kuhakikisha fursa hizo zinatekelezwa kwa kuzishirikisha nchi zote wananchama na kufikia Maendeleo Endelevu ya Mwaka 2030.

Vifo vya Kaunda, Magufuli na Dlamini

Mwenyekiti na Katibu Mtendaji wa SADC kwa pamoja walisema jumuiya hiyo imepata pigo la kuondokewa na viongozi watatu wa jumuiya hiyo ambao mmoja ni mwasisi wake, Rais Mstaafu wa Zambia, Kenneth Kaunda; Rais wa Awamu ya Tano wa Tanzania, Dk John Magufuli na Waziri Mkuu wa eSwatini, Ambrose Dlamini.

"Mchango wa viongozi hao kamwe hauwezi kusahaulika na historia itajiandika na kwamba wataendelea kuwa mioyoni mwa SADC na katika kuenzi mema yao, tutaendelea kujenga jumuiya yenye nguvu, viongozi hawa sio kwamba wameondoka bali wataendelea kuishi kwenye mioyo yetu,” alisema Rais Nyusi.

Rais Nyusi alisema SADC imeadhimisha miaka 40 ya kuundwa kwake na wanajivunia kujenga jamii yenye umoja na kwamba mafanikio zaidi yataonekana, huku wakishikamana kutatua changamoto zinazowakabili ili kufikia malengo yao ya maendeleo endelevu.

Waliohudhuria mkutano huo mbali ya Mwenyekiti Nyusi ni Rais Bostwana, Dk Mokgweetsi Masisi, Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, Rais Samia, Rais wa Zimbabwe, Dk Emmerson Mnangagwa, Rais wa Jamhuri wa Kidemokrasia ya Congo (DRC), Felix Tshisekedi, Waziri Mkuu wa Ufalme wa Lesotho, Dk Moeketsi Majoro na Naibu Waziri Mkuu wa eSwatini, Themba Masuku.

Nchi nyingine za SADC zilizoshiriki ni Madagascar, Comoro, Angola, Namibia, Zambia na Mauritius.

Chanzo: www.habarileo.co.tz