Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

SADC yakataa wito wa kutangaza dharura ya afya ya kipindupindu

Sadc Yakataa Wito Wa Kutangaza Dharura Ya Afya Ya Kipindupindu SADC yakataa wito wa kutangaza dharura ya afya ya kipindupindu

Thu, 1 Feb 2024 Chanzo: Bbc

Mawaziri wa afya kutoka muungano wa kanda ya kusini mwa Afrika, Sadc, wamekataa pendekezo la kutangaza kipindupindu kuwa dharura ya afya ya umma katika kanda.

Sylvia Masebo, mwenyekiti wa bodi ya Kituo cha Afrika cha Kudhibiti Magonjwa (CDC), Jumatano alisema nchi moja moja inapaswa kuamua kwa uhuru kama itatangaza mlipuko wa kipindupindu kama dharura ya kiafya au la.

Akizungumza wakati wa kikao cha ajabu cha CDC mjini Addis Ababa, Ethiopia, Bi Masebo, ambaye pia ni waziri wa afya wa Zambia, alizitaka nchi wanachama kuendeleza hatua za haraka ili kuzuia kuenea kwa mlipuko wa sasa.

Alisema mlipuko huo umeathiri takriban nchi 15 wanachama wa Sadc.

Zambia ni miongoni mwa nchi zinazopambana na mlipuko mbaya zaidi kuwahi kutokea katika miongo kadhaa, huku takriban vifo 600 na visa zaidi ya 16,000 vimeripotiwa tangu Oktoba mwaka jana.

Nchi imekumbwa na milipuko ya kipindupindu angalau mara 30 tangu 1977, huku shirika la kutoa misaada la WaterAid likisema mlipuko wa hivi punde ni mbaya zaidi tangu 2017.

Zimbabwe na Malawi pia zimeathiriwa na mlipuko wa sasa wa kipindupindu.

Viongozi wa Sadc wanatazamiwa kufanya mkutano wa kilele usio wa kawaida siku ya Ijumaa ili kutathmini hali ya kujiandaa na kukabiliana na milipuko ya kipindupindu.

Chanzo: Bbc