Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

SADC wakubaliana namna ya kukabili ugaidi

75638ec40dffd93c31517eeb2970f910.jpeg SADC wakubaliana namna ya kukabili ugaidi

Sun, 29 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

ASASI ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa (UN) zimekubaliana kuboresha mfumo utakao weka ulinzi bora na usalama ndani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Akithibitisha kuhusu mashirikiano ya mfumo wa kuimarisha ulinzi na usalama nchini DRC, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ambaye amemwakilisha Rais John Magufuli katika mkutano huo, alisema kuwa kamati ya utatu inayoshughulika na usalama ndani ya jumuiya ya SADC imekutana kwa dharura.

Lengo ni kuangalia namna ya kukabiliana na matishio ya ugaidi yanayotishia hali ya amani na usalama katika nchi zilizopo ukanda wa SADC ikiwemo Msumbiji, Congo DRC na Tanzania.

"Tumeangalia kwa undani mapendekezo mapya ya mfumo wa ulinzi katika enep la DRC,” alisema Samia.

Alisema kupitia mkutano huo pia limejadiliwa suala la hali halisi ya usalama ndani ya nchi wanachama ndani ya SADC na kuona jinsi ya kutumia usalama kwa ajili ya kujenga uchumi wa ukanda wetu wa kusini mwa Afrika

Rais wa Botswana, Dk Mokgweetsi Masisi ambae pia alikuwa Mwenyekiti wa Mkutano huo amezipongeza nchi za Tanzania pamoja na Visiwa vya Shelisheli kwa kufanya uchaguzi huru, haki na amani na kuzitaka nchi nyingine kuiga mfano huo wa kuwa na demokrisia ya uhuru, amani na haki.

"Matokeo ya uchaguzi huo ni mfano mzuri kwetu sisi kama nchi wanachama wa SADC kujifunza mfano kutoka kwa wenzetu," alisema Masisi.

Alisema pamoja kufanya chaguzi huru,za haki na za amani, kuna mambo ambayo yamekuwa yakijitokeza katika ukanda wa SADC kama vile, ugaidi, uhalifu wa kimtandao na vikundi vya waasi jambo ambalo limesababisha wakuu wa nchi na serikali kukutana Gaborone, Botswana.

"Mtakumbuka kuwa katika mkutano wetu wa SADC uliofanyika Agosti mwaka huu tulitoa ripoti iliyoonesha kuwa na baadhi ya nchi kuna ugaidi kwahiyo kuna haja ya kuungana pamoja na kuhakikisha kuwa vikundi hivi vya kigaidi vinatokomezwa katika ukanda wetu wa SADC," alisema.

Pamoja na mambo mengine, Asasi ya SADC ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama inawajibika kukuza amani na usalama katika eneo la SADC na pia ina wajibu wa kuongoza na kuzipatia nchi wanachama mwongozo kuhusu mambo ambayo yanatishia amani, ulinzi na usalama.

Ni mara ya kwanza kwa wakuu wa nchi na Serikali wa SADC – TROIKA kukutana ana kwa ana tangu ulipotokea ugonjwa wa homa kali ya mapafu (Covid-19).

Pamoja na Makamu wa Rais, Samia, mkutano huo ulihudhuriwa na, Rais wa Botswana , Masisi, Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa, Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, Rais wa Malawi, Lazarus Chikwera, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Felix Tshisekedi. Wengine ni Waziri wa Ulinzi wa Msumbiji, Jaime Neto aliyemwakilisha Rais Filipe Nyusi.

Chanzo: habarileo.co.tz