Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

SADC kutoa majeshi kukabili ugaidi Msumbiji

Fd824985efd810656ccf57f0d4178789.PNG SADC kutoa majeshi kukabili ugaidi Msumbiji

Sat, 26 Jun 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

NCHI 14 za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) zimeamua kushirikiana kikamilifu kuisaidia Msumbiji katika kupambana na kukomesha ugaidi ulioibuka katika Jimbo la Cabo Delgado nchini humo.

Akizungumza jijini Dodoma baada ya kufungua Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula amesema hilo ni miongoni mwa maazimio matatu yaliyofikiwa katika mkutano wa dharura wa viongozi wa SADC uliofanyika Msumbiji.

Katika mkutano huo ambao Rais Samia Suluhu Hassan alihudhuria kwa mara ya kwanza, Mulamula alisema viongozi hao waliweka maazimio matatu likiwemo la kujikinga na covid-19 na hali ya chakula katika ukanda.

“Kutokana na hali ya usalama katika jimbo la Cabo Delgado kuwa tete, viongozi wa SADC kwa umoja wao wameazimia kuweka mpango wa pamoja wa kuisaidia Msumbiji katika kupambana na magaidi,” alisema Balozi Mulamula.

Nchi hizo zimekubaliana kupambana na magaidi hao kwa kupeleka vikosi vya kijeshi pamoja na kutenga bajeti kwa ajili ya kusaidia nchi hiyo inayopakana na Tanzania upande wa Kusini.

Magaidi hao walianza mashambulizi 2017 huko Mocimboa da Praia na kuenea kwenye maeneo makubwa ya jimbo la Cabo Delgado.

Balozi Mulamula alisema katika kujiandaa kusaidia nchi hiyo, kikao cha Mawaziri wa Mambo ya Nje kitafanyika Juni 28, mwaka huu kwa ajili ya kuangalia ni namna gani kila nchi itachangia askari pamoja na bajeti ya kusaidia askari hao kupambana na magaidi hao.

Wakati nchi za SADC zikitaka kuisaidia kwa muda wote vikosi vya usalama vya Msumbiji vimekuwa zikiendelea kupambana na kundi hilo kurudisha udhibiti wa bandari muhimu katika jimbo lenye utajiri wa gesi Kaskazini mwa Msumbiji.

Chanzo: www.habarileo.co.tz