Serikali ya Rwanda imepinga ripoti ya kundi la wataalamu wa umoja wa mataifa iliyosema kwamba Rwanda ilishambulia vikosi vya DR Congo na kusaidia waasi wa M23.
Taarifa iliyotolewa na Msemaji wa serikali ya Rwanda Yolande Makolo inasema kuwa ripoti hiyo inalenga kuzubaisha dunia kuhusu suala la M23 ambalo Rwanda inasema linahusu DRC yenyewe na kwamba ikiwa suala la waasi wa FDLR wanaopinga Rwanda halitatatuliwa usalama katika eneo la maziwa makuu utaendelea kuwa shida.
Katika taarifa iliyotolewa na msemaji wa serikali ya Rwanda, Yolande Makolo, inasema kuwa Rwanda haizungumzii ripoti hiyo ambayo bado haijaidhinishwa rasmi.
Lakini inaendelea kusema kwamba "mradi swala la waasi wa FDLR, ambao wanafanya bega kwa bega na jeshi la DR Congo, halitazingatiwa kuwa kubwa vya kutosha na kutatuliwa, usalama katika eneo la Maziwa Makuu hautapatikana."
Katika Tangazo hilo msemaji wa serikali ya Rwanda amekumbusha mabomu yaliyorushwa nchini Rwanda kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kusema kwamba kulikuwa na uchunguzi na ilijumuishwa katika ripoti ya wataalamu wa UN iliyochapishwa mnamo mwezi Juni.
Ilisema: "Rwanda ina haki ya kisheria ya kulinda uhuru wake na watu, sio tu kungoja hatari ije."
Shutuma kuwa Rwanda ilishambulia vikosi vya DRC
Kundi la wataalamu wa Umoja wa Mataifa linasema lina "ushahidi wa kutosha " kwamba jeshi la Rwanda limekuwa likipigana pamoja na waasi wa M23 mashariki mwa DR Congo na kuwapa silaha.
Taarifa hizo zimo katika ripoti iliyoainishwa yenye kurasa 131 ambayo mashirika ya Reuters na AFP yalisema yaliipata siku ya Alhamisi.
Serikali ya Rwanda imekuwa ikikanusha kusaidia M23, kundi hili pia linasema kuwa halipati msaada wowote kutoka Rwanda.
Kundi hilo la Umoja wa Mataifa linasema kuwa "limeona ushahidi mkubwa wa mashambulizi ya kijeshi yaliyofanywa na Jeshi la Ulinzi la Rwanda katika Wilaya ya Rutshuru kati ya Novemba 2021 na Julai 2022".
Waasi wa M23 sasa wanadhibiti baadhi ya maeneo ya eneo la Rutshuru na mji mdogo wa Bunagana kwenye mpaka wa Uganda na DR Congo.
Kulingana na Reuters ,Ripoti hiyo inasema kuwa wanajeshi wa RDF walifanya mashambulizi pamoja na M23 dhidi ya vikosi vya DR Congo na makundi yenye silaha, na kuwapa M23 silaha,sare za kijeshi na risasi.
Ripoti hii inasema kuwa baadhi ya wanajeshi wa DR Congo walisaidia na kupigana bega kwa bega na waasi wa FDLR, wanaopinga serikali ya Rwanda.
AFP inarudia yaliyomo katika ripoti hii ambayo inasema kwamba mnamo Mei 25 kambi kubwa ya kijeshi ya Rumangabo huko Kivu Kaskazini ilishambuliwa kwa risasi na bunduki kubwa na ndogo na Kwamba hili lilikuwa ni "shambulio la pamoja" la M23 na jeshi la Rwanda, baada ya takriban wanajeshi 1,000 wa Rwanda kuvuka hadi DR Congo siku iliyotangulia.
Kulingana na shirika la AFP ,Kabla ya shambulio dhidi ya mji wa Bunagana, na siku halisi, jeshi la Rwanda lilikuwa karibu, ripoti hii ni kwa mjibu wa picha za ndege zisizo na rubani za MONUSCO, mashahidi, na video na picha za watu wa kawaida.
Taarifa ya serikali ya Rwanda imesema kwamba tatizo la M23 "linajulikana sana kama tatizo la DRC, ambalo wanataka kulifanya kama mzigo na kuuweka kwa nchi nyingine".
Kabla ya shambulio la Bunagana, na siku hiyo yenyewe, jeshi la Rwanda lilikuwa karibu, ripoti inasema,Ushahidi ni kutokana na picha za ndege zisizo na rubani za MONUSCO, mashahidi, na picha za raia, kulingana na shirika la AFP.
Viongozi wa makundi mbalimbali ya waasi waliwaambia wataalamu wa Umoja wa Mataifa kwamba jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limewapa silaha na risasi "mara nyingi", kulingana na ripoti ya AFP.
Jeshi la DRC limekanusha mara kwa mara kusaidia FDLR au kushirikiana na waasi wengine.
Uhusiano kati ya Rwanda na DR Congo umekuwa matatani tangu mwishoni mwa mwaka jana wakati kundi la M23 lilipopata nguvu baada ya miaka 10 wanachama wake walikimbilia Uganda na Rwanda.