Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rwanda yakumbuka Mkapa alivyoiokoa mauaji ya kimbari

4bfe9a9c2f6fa7ef465e2798850ac094 Rwanda yakumbuka Mkapa alivyoiokoa mauaji ya kimbari

Tue, 28 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

SERIKALI ya Rwanda imesema kuondoka kwa Rais wa Awamu ya Tatu Hayati Benjamin Mkapa ni pigo kubwa kwa wananchi wa Rwanda na taifa hilo kutokana na mchango mkubwa alioutoa nchi hiyo ilipopitia kipindi kigumu cha mauaji ya kimbari mwaka 1994.

Balozi wa Rwanda nchini Tanzania, Charles Karamba aliyasema hayo alipokuwa akifanya mahojiano na waandishi wa magazeti ya serikali ya Daily News na Habarileo katika ofisi zake zilizopo Oysterbay, Jijini Dar es Salaam.

Alisema Rais Mkapa alipoingia madarakani mwaka 1995, aliikuta Rwanda katika matatizo makubwa ya kuuana na wananchi wa taifa hilo kukimbilia nchini hapa kunusuru maisha yao.

Balozi Karamba alisema kwa hekima na uwezo mkubwa wa Mkapa alisaidiana na wazalendo wa Rwanda wakiongozwa na Rais Paul Kagame kuwanusuru wananchi wa Rwanda na kiuwahifadhi waliokimbilia nchini Tanzania.

“Baada ya hali kutengamaa Rwanda mwaka 1996, Mkapa aliwaruhusu wananchi hao kurejea Rwanda kushirikiana na viongozi wao kuijenga nchi kiuchumi na kijamii,” alisema Balozi Karamba.

Alisema baada ya Mkapa kuingia madarakani aliisaidia Rwanda kisiasa kuhakikisha inakuwa na amani ya kudumu ili kuruhusu maisha ya kawaida kuendelea ambapo wakimbizi waliokuwa nje ya nchi walirudi kwa hiari yao. Balozi Karamba alisema machafuko ya mwaka 1994 yalisababisha wananchi 500,000 kukimbia nchi yao na kuja Tanzania.

Alisema Serikali ya Rais Mkapa ilijitolea kuwahudumia kuwapa wakimbizi mahitaji yote muhimu kwa afya yao ikiwa ni pamoja na maji, hospitali na elimu.

Alisema Rais Mkapa ndiye kiongozi wa kwanza Afrika na duniani kuona na kuamini kuwa Rwanda ina amani na utulivu, akawaruhusu wakimbizi wote kurudi nyumbani kwao.

“Rais Mkapa wakati ule alitusaidia kuunganisha Wanyarwanda kutokana na mgawanyiko mkubwa uliojitokeza kutokana na mauaji ya kimbari yaliyotokea, alituunganisha kisiasa na kijamii,” aliongeza Balozi Karamba.

Alisema Mkapa wakati huo akiwa Rais wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), alishirikiana na Rais Paul Kagame kukijenga vizuri chama tawala cha Rwanda cha Rwanda Patriotic Front (RPF) na ushirikiano wa RPF na CCM uliwaunganisha Wanyarwanda kisiasa na kuwa kitu kimoja.

Balozi Karamba alisema hata baada ya Mkapa kustaafu, aliendelea kuwa karibu na wananchi wa Rwanda, kuwa karibu na Rais Kagame na pia katika shughuli za kiuchumi na kijamii.

“Katika uongozi wake, Rais Mkapa aliwahimiza viongozi wa Rwanda kuweka maslahi ya wananchi mbele ili kusaidia kutatua kero zao na kuwawezesha kiuchumi, hilo ni jambo ambalo kama Wanyarwanda hatutalisahau,” aliongeza Karamba.

Chanzo: habarileo.co.tz