Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rwanda kutumia dola milioni 100 kukarabati miundombinu

Tope Rwanda Mafuriko Rwanda kutumia dola milioni 100 kukarabati miundombinu

Mon, 8 May 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali ya Rwanda imesema, imetenga karibu dola milioni 100 kukarabati miundombinu iliyoharibika kufuatia mafuriko makubwa na maporomoko ya ardhi wiki hii ambayo yalisababisha vifo vya watu 131 na kubomoa maelfu ya nyumba.

Zaidi ya watu 9,000 wameachwa bila makazi baada ya mito ya matope kusomba vijiji na kukata mawasiliano ya barabara kufuatia mvua kubwa iliyonyesha katika maeneo kadhaa ya taifa hilo dogo la Afrika Mashariki.

Waziri wa Masuala ya Dharura na ya Hatari Marie-Solange Kayisire amesema, mmoja wa waliojeruhiwa katika maafa hayo alifariki dunia hospitalini siku ya Jumamosi na kuifanya idadi ya walioaga dunia katika janga hilo kufikia 131.

Kayisire amewaeleza waandishi wa habari mjini Kigali kuwa, wangali wanaendelea kumtafuta mtu mmoja ambaye hajulikani aliko.

"Zaidi ya watu 9,000 wamebaki bila makazi kutokana na janga hili", ameongeza waziri huyo anayehusika na masuala hatari na ya dharura.

Skuli zipatazo 50 zimebomolewa pamoja na miundombinu muhimu ikiwa ni pamoja na barabara, madaraja, vituo vya maji na gridi ya umeme katika moja ya majanga makubwa zaidi ya kimaumbile kuwahi kutokea nchini Rwanda.

Afrika Mashariki mara nyingi huathiriwa na hali mbaya ya hewa wakati wa misimu ya mvua.

Mnamo Mei 2020, watu wapatao 65 walifariki dunia nchini Rwanda kutokana na mvua kubwa iliyonyesha katika eneo hilo. Aidha, watu zaidi ya 200 walipoteza maisha kutokana na mafuriko na maporomoko ya ardhi katika miezi minne ya kwanza ya mwaka 2018.

Wiki hii pia zaidi ya watu 170 walifariki baada ya mvua kubwa na mafuriko kulikumba eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Wataalamu wanasema, matukio ya hali mbaya ya hewa yanatokea mara kwa mara na kwa nguvu kubwa katika eneo hilo la mashariki ya Afrika kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres siku ya Jumamosi alitoa salamu za rambirambi kwa wahanga wa mafuriko makubwa yaliyotokea katika nchi za Rwanda na DRC.

"Hiki ni kielelezo kingine cha kuongezeka kasi ya mabadiliko ya tabianchi na athari zake mbaya kwa nchi ambazo hazijahusika kwa namna yoyote ile katika kuchangia ongezeko la joto duniani," alisema Guterres alipokuwa ziarani nchini Burundi..

Chanzo: www.tanzaniaweb.live