Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rwanda: Rais Kagame afanya mabadiliko makubwa katika jeshi

Rwanda: Rais Kagame Afanya Mabadiliko Makubwa Katika Jeshi Rwanda: Rais Kagame afanya mabadiliko makubwa katika jeshi

Tue, 6 Jun 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Rais wa Rwanda Paul Kagame amewateua wakuu wapya wa kijeshi na kijasusi katika mojawapo ya mabadiliko makubwa ya kiusalama katika miaka ya hivi karibuni.

Juvénal Marizamunda sasa ndiye Waziri mpya wa Ulinzi wa Rwanda, huku Luteni Jenerali Mubarakh Muganga akiwa mkuu mpya wa majeshi ya Rwanda (RDF).

Bwana Marizamunda, aliyechukua nafasi ya Meja Jenerali Albert Murasira katika wizara ya ulinzi, alikuwa Mkuu wa Jeshi la Magereza.

Luteni Jenerali Muganga, aliyechukua nafasi ya Jenerali Jean Bosco Kazura, alikuwa kamanda mkuu wa jeshi la ardhini.

Meja Jenerali Vincent Nyakarundi, ambaye hapo awali alikuwa mkuu wa upelelezi wa kijeshi, alichukua nafasi ya Luteni Jenerali Muganga kama kamanda mkuu wa jeshi la ardhini.

Haya ni mabadiliko ambayo hayajitokezi mara kwa mara katika jeshi la Rwanda ambapo waziri wa ulinzi anabadilishwa kabla hajatumikia miaka mitano, na mkuu wa majeshi anabadilishwa kabla hajatimiza miaka minne kwenye wadhifa huo na wanaondolewa kwa wakati mmoja.

Sababu ya mabadiliko haya haikuwekwa wazi katika tangazo lililotolewa na ofisi ya rais Jumatatu usiku, na katika mabadiliko hayo ambayo yamewahi kutokea, wakati mwingine Rais Kagame mwenyewe ndiye alisisitiza kwa nini alifanya mabadiliko hayo.

Miongoni mwa mabadiliko hayo, Kanali Francis Regis Gatarayiha aliteuliwa kuwa kaimu mkuu wa ujasusi wa kijeshi, huku Jean Bosco Ntibitura akiwa mkurugenzi mkuu wa usalama wa taifa katika Huduma ya Kitaifa ya Ujasusi (NISS).

Brigedia Jenerali Evariste Murenzi aliteuliwa kuwa mkuu wa jeshi la magereza , akichukua nafasi ya Marizamunda.

Meja Jenerali Alex Kagame amechukua wadhifa wa kamanda wa operesheni za kijeshi nchini Msumbiji, wakati Kanali Théodomir Bahizi atahusika na maswala ya vita nchini Msumbiji.

Tangu mwezi wa Julai mwaka 2021, Rwanda imetuma wanajeshi na polisi nchini Msumbiji - kwa ombi la serikali ya nchi hiyo -kupambana dhidi ya watu wenye itikadi kali wanaodai kuwa Waislamu waliokuwa wameteka maeneo mengi ya jimbo la Cabo Delgado kaskazini mwa nchi hiyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live