Mvutano wa kidiplomasia kati ya Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo unazidi kupamba moto, baada ya Kigali kuituhumu Kinshasa kwamba, inavuruga jitihada za kikanda zinazoendelea za kuleta amani mashariki mwa nchi hiyo.
Mgogoro baina ya mataifa hayo mawili jirani umeingia katika hatua mpya baada ya serikali ya Kigali kudai kwamba, Jamhuuri ya Kidemokrasia ya Congo ilikuwa inajiandaa kwa vita kwa kuwaajiri mamluki wa kigeni.
Wakati Rwanda ikitoa tuhuma hizo, serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo nayo imeendelea kuinyooshea kidole cha lawama Kigali kwamba, ndio mvurugaji wa amani na usalama mashariki mwa DRC.
Uhusiano kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Rwanda umefikia hatua ya chini kabisa katika miezi ya hivi karibuni.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inaituhumu jirani yake mdogo Rwanda kuwa inaliunga mkono kundi la waasi wa M23, madai ambayo yamekanushwa na Rwanda, lakini yanaungwa mkono na Marekani, Ufaransa, Ubelgiji na wataalamu wa Umoja wa Mataifa.
Wanamgambo hao wameteka eneo la mashariki mwa DRC lenye hali tete na lenye utajiri wa madini katika miezi ya hivi karibuni, na hivyo kuzusha mvutano kati ya serikali ya Kinshasa na Rwanda.
Ripoti iliyotolewa hivi karibuni na wataalamu huru wa Umoja wa Mataifa ilieleza kuwa, jeshi la Rwanda lilihusika kwenye "operesheni za kijeshi" dhidi ya jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika maeneo yanayokabiliwa na machafuko mashariki mwa DRC.