Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ruto na Raila kutoana jasho kinyang'anyiro cha nyadhfa za Maspika

Bunge La Kenya.png Ruto na Raila kutoana jasho katika kinyang'anyiro cha nyadhfa za Maspika

Thu, 8 Sep 2022 Chanzo: BBC

Rais mteule William Ruto na kiongozi wa Azimio Raila Odinga watamenyana hii leo Alhamisi kila mmoja akitafuta kudhibiti Bunge.

Wanachama waliochaguliwa na kuteuliwa wa Bunge la Seneti na Bunge la Kitaifa wanakutana kwa mara ya kwanza leo ili kuapishwa na kuwachagua maspika na manaibu wao.

Vikao vya mabunge hayo mawili vinaanza saa tatu asubuhi.

Hapo jana Jumatano, miungano ya Kenya Kwanza na Azimio ilifanya mikutano yao ambapo waliwachagua wanaowapendekeza kwa nyadhifa zenye ushawishi mkubwa.

Katika Bunge la Kitaifa, Muungano wa Azimio unaoongozwa na Raila Odinga ulihitimisha kwamba aliyewahi kuwa Spika wa Bunge la Kitaifa Kenneth Marende na Farah Maalim kuwania nafasi za Spika na Naibu wake mtawalia.

Upande wa muungano wa Kenya Kwanza unaoongozwa na William Ruto, umewachagua mkuu wa Ford Kenya Moses Wetangula na Gladys Shollei kwa nyadhifa za Spika na Naibu Spika.

Katika Bunge la Seneti, muungano wa Kenya Kwanza wa Ruto ulimchagua aliyekuwa Gavana wa Kilifi Amason Kingi na Seneta wa Meru Kathuri Murungi kwa nyadhifa za Spika na Naibu Spika mtawalia.

Muungano wa Azimio, kwa upande wake ukamchagua kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka kuwania Spika wa Bunge la Seneti na Seneta Mteule wa Kilifi Stewart Madzayo kuwania Naibu Spika.

Nafasi ya Spika ina umuhimu mkubwa wa kisiasa kwa muungano wowote ule kwa sababu mhusika anakuwa wa tatu katika uongozi wa nchi.

Katiba inasema kwamba mtu lazima apate theluthi mbili ya kura ili kuchaguliwa spika katika duru ya kwanza ya upigaji kura, au apate wingi wa kura katika duru inayofuata.

Hata hivyo, upigaji kura ni kwa njia ya siri kwa hivyo, kando na kufuata mkondo wa muungano, wanachama wanaweza kupiga kura kulingana na ushawishi wa wagombea.

Wabunge 12 waliopendekezwa wa Bunge la Kitaifa na 20 waliopendekezwa katika Bunge la Seneti, ambao pia watashiriki katika kura hiyo, walitangazwa kwenye gazeti rasmi la serikali jana jioni.

Pia wabunge wanne waliochaguliwa katika maeneo ambayo uchaguzi wao uliahirishwa pia walitangazwa kwenye gazeti la serikali.

Chanzo: BBC