Rais wa Kenya, William Ruto amevunja kitengo maalum cha Polisi (SSU), kilichokuwa kikihudumu chini ya afisi ya Mkurugenzi mkuu wa Ujasusi DCI nchini Kenya, ikiwa ni ni sehemu ya mabadiliko ya uongozi huku utawala mpya ukipania kurekebisha usimamizi wa idara ya usalama nchini humo.
Ruto amefikia uamuzi huo, baada ya kupokea ripoti ya uchunguzi kuhusu kutoweka kwa raia wawili wa India na mwenyeji wao aliyekuwa dereva wa gari huku akisema, kitengo hicho ndicho kilichohusika pakubwa na mauaji ya kiholela na kupotea kwa watu ambão miili yao baadaye ilipatikana maeneo tofauti nchini kama vila mto Yala.
Ripoti hiyo ilipendekeza kuvunjiliwa kwa kitengo hicho ili kuruhusu uchunguzi kukamilika kabla ya faili kuwasilishwa kwa mkurugenzi mkuu wa mashtaka nchini kenya, na Ruto anasema, “Tuna mpango wa kuimarisha usalama nchini Kenya ili kuzuia aibu ya Wakenya kuuawa na maafisa wa polisi na miili yao kutupwa katika Mto Yala na kwengine.”
Kitengo hicho, kilipewa jukumu la kushughulikia uhalifu wa hali ya juu ikiwemo wa kutumia silaha, utekaji nyara na wizi wa magari katika jiji na kaunti zinazozunguka mji wa Nairobi , lakini majukumu yao mara kwa mara yaliongezeka zaidi ya mji wa Nairobi.
Nchini Kenya, kumekuwa na tuhuma kwamba polisi wamekuwa wakihusika na vifo na kupotea kiholela kwa Wakenya ambapo wanaharakati wa haki za binadamu wametaka uchunguzi ufanyike.
Mapemamo Aprili na Mei 2019, Shirika la haki za kibinadamu la Human Rights Watch lilihoji watu 35 wakiwemo mashahidi, wanafamilia wa waathiriwa, madaktari na wafanyakazi wa kijamii, wanaharakati, na wafanyakazi wa polisi akiwemo msemaji wa polisi jijini Nairobi juu ya shutuma mbalimbali zilizoelekezwa kwa Polisi hao sambamba na maswali juu matukio ya kiuhalifu.