Wakati matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika jana, Jumatano Agosti 9, 2022 yakiendelea kutangazwa, mgombea wa Kenya Kwanza, William Ruto ameipongeza Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC) kwa kuendesha vema mchakato huo.
Kupitia ukurasa wake wa twitter, Ruto ambaye pia ni Naibu Rais, ameandika: “Siku kama ya leo (Agosti 11, 2022) miaka mitano baadaye, Agosti 10, 2027, Wakenya watapanga mstari tena kutekeleza haki hii ya kidemokrasia kwa amani”.
“Tumeshuhudia usimamizi bora uliofanywa na IEBC katika uchaguzi wa Agosti 9, 2022. Hongera,” ameandika.
Ruto ametoa kauli hiyo wakati matokeo ya awali yakionyesha anaongoza kwa asilimia 51.15 kwa kura 860,688 huku mpinzani wake Raila Odinga wa Azimio la Umoja akiwa na asilimia 48.23 sawa na kura 811,548.
Wagombea wengine wa nafasi hiyo ni George Wajackoyah wa chama cha Roots mwenye asilimia 0.41 sawa na kura 6,975 na David Waihiga wa Agano akiwa na asilimia 0.21 sawa na kura 3,486.