Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ruto abana safari za maofisa wa Serikali yake

Ruto Akataa Nyongeza Ya 14% Ya Mshahara Ruto abana safari za maofisa wa Serikali yake

Wed, 4 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Rais wa Kenya, William Ruto amezuia safari zisizo za lazima kwa maofisa wa Serikali akiwa na lengo la kubana matumizi.

Ruto anatumia mbinu hiyo ya kurekebisha mwongozo wa safari, sawa na ilivyokuwa kwa awamu ya tano nchini Tanzania, ambapo miezi kadhaa baada ya Rais John Magufuli kuingia madarakani, alichukua maamuzi kama hayo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mkuu wa Utumishi wa Umma, Felix Koskei iliyotolewa jana, Serikali haitarejesha tena gharama zilizotumika kwa ziara, safari za mafunzo na mipango inayohusiana na kuwajengea uwezo, utafiti, mikutano ya kitaaluma na kongamano yanazofanywa na viongozi wa Serikali.

Matukio mengine yatakayoathirika ni pamoja na makongamano na mikutano ya ushiriki wa jumla, matukio ya kando na maonyesho, na mikutano ama matukio ya kamati na vyama, matukio yaliyofadhiliwa ambayo yanahitaji nyongeza ya bajeti ya kulala na kusafiri

Taarifa hiyo inafafanua, maofisa wataruhusiwa tu kuwa nje ya nchi kwa muda usiozidi siku saba, zikiwemo tarehe za kusafiri.

Koskei amesema hatua hiyo ni sehemu ya mikakati ya sera ya fedha ya ‘Kenya Kwanza’ inayokusudia kuimarisha matumizi ya rasilimali inayopatikana kwa maendeleo ya kitaifa na kaunti.

"Taasisi za umma zinazotaka kusafiri na kushiriki katika hafla zozote zilizo hapo juu zinatakiwa kuomba ushiriki wa mtandaoni pale zinapopatikana kwa kushirikisha Wizara ya Mambo ya Nje na Diaspora ili kuhakikisha ushiriki wa moja kwa moja,” imenukuu sehemu ya taarifa hiyo ya Koskei.

Agosti, mwaka huu Naibu Rais Rigathi Gachagua alikemea baraza la mawaziri na makatibu wakuu wenye utamaduni na tamaa kubwa za kusafiri nje, akisema baadhi ya maofisa hubadilisha nguo katika viwanja vya ndege wanaposafiri kwenda nchi zingine.

Julai, Serikali ilipitia miongozo ya safari za nje ya baraza la mawaziri na makatibu wakuu pamoja na wenyeviti na watendaji wakuu wa mashirika ya Serikali.

kibano cha waraka mpya

Mwongozo huo mpya unaweka idadi ya siku ambazo katibu wa baraza la mawaziri, katibu mkuu au ofisa mtendaji mkuu wa shirika la serikali anaweza kuwa nje ya nchi kwa siku saba, siku 15 katika kila baada ya miezi mitatu na siku 45 kwa mwaka.

Waraka huo unasema pale ambapo katibu wa baraza la mawaziri ataambatana na angalau mmoja wa wajumbe, lazima awe ofisa wa kiufundi aliyebobea katika mada ya itakayojadiliwa ziarani bila wasaidizi wa usalama au wa kibinafsi au ofisa wa usafirishaji isipokuwa kama amewezeshwa.

Ujumbe wa katibu mkuu hautazidi watu wawili ikiwa ni pamoja na katibu mkuu, wenye mahitaji sawa na CS. Ujumbe unaohusisha baraza la mawaziri na katibu mkuu utawekewa kikomo cha watu watatu,”imeeleza taarifa ya mwongozo huo.

"Inasisitizwa makatibu wa baraza la mawaziri na makatibu wakuu wa wizara hizo hawapaswi kusafiri nje ya nchi kwa wakati mmoja isipokuwa ushirikiano wa kigeni unaohitaji hivyo," waraka huo umenukuu.

Aidha, mwenyekiti au ofisa mkuu mtendaji wa shughuli za sekta ya umma atalazimika kusafiri peke yake, isipokuwa kama watakuwa sehemu ya ujumbe wa baraza la mawaziri au katibu mkuu bila usalama, wasaidizi wa kibinafsi au maofisa wa usafirishaji, isipokuwa kama watakuwa wamewezeshwa.

Aidha, ujumbe unaoongozwa na mwenyekiti au ofisa mtendaji mkuu wa tume za kikatiba na ofisi huru hautazidi watu wawili akiwemo mkuu wa ujumbe bila wasaidizi wa usalama au wasaidizi wa kibinafsi au maafisa wa usafirishaji isipokuwa kama wamewezeshwa.

Ujumbe unaoongozwa na magavana hautazidi watu watatu, akiwemo gavana kama mkuu wa wajumbe. Pale ambapo mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Kata atasafiri kwa niaba ya gavana, atasafiri peke yake.

Waraka huo pia umesimamisha uidhinishaji wote kwa watumishi wengine wa serikali uliotolewa na makatibu wakuu na maafisa wakuu watendaji, isipokuwa kwa usafiri unaohusiana na likizo na uwakilishi rasmi wa katibu mkuu husika au mkurugenzi mtendaji wa wakala.

Hatua hizo za kubana matumizi pia zitaathiri wajumbe wanaoandamana na rais, naibu wake, mke wa rais na katibu wa kabineti ya waziri mkuu.

Kwa mujibu wa waraka huo, usafiri huo utaidhinishwa tu kwa ma0fisa wenye jukumu la moja kwa moja katika shughuli zilizopangwa au mipango ya wakuu.

"Wizara ya Mambo ya Nje na Masuala ya Diaspora inaelekezwa kurekebisha na kupunguza kwa asilimia 50 idadi ya watumishi wanaoandamana na kila mmoja wa wakuu," umenukuu waraka huo.

Agizo hilo linahusisha kwa Hazina ya Kitaifa na Mipango ya Kiuchumi, itakayolazimika kurekebisha bajeti zote za safari za nje na za ndani kwa asilimia 50.

Wizara ya Mambo ya Nje itapunguza utoaji wa jumla wa mialiko kwa taasisi za serikali na kuhakikisha ushiriki wa taasisi muhimu pale tu inapobidi.

Aidha, Viza za kusafiri na nyaraka nyingine zitaongezewa muda tu kwa safari zinazohusisha shughuli za Serikali.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live