Wapiganapo mafahari wawili, ziumiazo ni nyasi, huenda huu ukawa msemo sahihi zaidi kwa kile kinachoendelea nchini Kenya, kufuatia maandamano ya mara kwa mara ya upinzani, dhidi ya Serikali ya Rais William Ruto tangu kuapishwa kwake mnamo Septemba 13, 2022.
Mvutano kati ya Kiongozi Mkuu wa Upinzani nchini humo Raila Odinga na Serikali ya Rais Ruto umekuwa shubiri hadi kwa wananchi wa kawaida kufuatia madhara ya maandamano yanayoongozwa na upinzani nchini humo.
Ushawishi mkubwa alionao Raila Wakenya, umefanya upinzani kati yake na Rais Ruto kuwa mkubwa na kufanya muitikio wa kuipinga Serikali nchini humo kuongezeka siku hadi siku.
Kiuhalisia, jambo hilo limedhihirika katika maandamano ya kupinga kuongezeka kwa gharama za maisha nchini humo, ambayo kimsingi yanaongozwa na kinara huyo wa Azimio la Umoja, Raila ambaye ni mtoto wa mwanamapinduzi wa nchi hiyo na aliyewahi kuwa Makamo wa Rais Jaramogi Oginga Odinga.
Kwa takriban wiki mbili sasa tangu kurejea kwa maandamano ya upinzani nchini humo, tayari madhara makubwa yameshuhudiwa ikiwemo watu kupoteza maisha, uharibifu wa mali na hasara katika biashara mbalimbali.
Waziri wa Uchukuzi nchini humo Kipchumba Murkomen amesema takriban Sh70 milioni za Kenya sawa na Sh1.2 bilioni za Tanzania zinahitajika ili kufanya ukarabati katika miundombinu ya barabara iliyoharibiwa wakati wa maandamano ya Jumatano wiki iliyopita.
Umoja wa Sekta binafsi nchini Kenya (Kepsa) ulisema kuwa sekta binafsi inapoteza wastani wa Sh3 bilioni za Kenya sawa na Sh51.7 billioni za Tanzania kwa siku kutokana na maandamano nchini humo.
Hiyo ni kutokana na maandamano hayo kusababisha shughuli za kiuchumi kusuasua nchini humo na kusababisha hasara kwenye biashara kutokana na ama kufungwa kufuatia sababu za usalama, au uporaji unaofanyika wakati wa maandamano hayo.
Mpaka sasa takribani watu 15 wamepoteza maisha kufuatia maandamano ya siku mbili pekee, (Ijumaa Julai 5, na Jumatano Julai 7) huku askari na raia wakijeruhiwa.
Hofu ya umasikini na madhara mengine kama vifo inazidi kuongezeka kutokana na mwitikio wa maandamano kuwa mkubwa kila uchao huku kupanda kwa gharama za maisha kukitajwa kuchagiza ongezeko hilo na si ushawishi pekee wa Odinga.
Hata hivyo mpaka sasa hakuna dalili ya maridhiano baina ya pande hizo mbili ambapo kiongozi huyo wa upinzani akiwa ameitisha maandamano ya siku tatu mfululizo kuanzia leo Jumatano huku Rais Ruto pia akiapa kukomesha maandamano hayo.
Wadau mbalimbali wanaonya kwamba maandamano yaliyopangwa kufanyika kwa siku tatu mfululizo nchini humo kuanzia Kesho Julai 19 huenda yakalitumbukiza taifa hilo katika umasikini na madhara mengine kama vifo na athari kwa nchi jirani pia.
Mwanadiplomasia ya Uchumi kutoka chuo kikuu cha Dar es Salaam, Prof Kitojo Wetengere alisema athari za maandamano hayo si kwa Kenya tu bali hata nchi jirani ikiwemo Tanzania zinaweza kuathirika na maandamano hayo.
“Athari hizo ni pamoja na wakimbizi kwenye mataifa ya jirani japo vifo ni matokeo mengine ambapo huenda idadi ikawa kubwa zaidi kuliko ile iliyotokea katika wiki mbili Zilizopita,” alisema Prof Wetengere.
Prof Wetengere alisema Tanzania ina jambo la kujifunza kwani mara nyingi Watanzania wamekuwa wakililia demokrasia na uhuru wa kuandamana jambo ambalo si baya lakini kusipokuwa na mfumo mzuri wa usimamizi wa maandamano, wanasiasa wenye agenda binafsi za kisiasa wanaweza kuwatumia wananchi na vijana kwa maslahi yao binafsi.
“Uhuru una faida na hasara zake. Ili kuepusha athari hizo mbaya, ni vizuri mifumo ya uchaguzi iwe ya haki na kusiwepo na makundi ya watu wasioridhika na mchakato mzima wa uchaguzi,” alisema Prof Wetengere.
Aidha alionya kwamba endapo maandamano yakiendelea huenda Taifa hilo likatumbukia katika anguko la kiuchumi na kuongeza umasikini nchini humo.
“Nguvu kubwa inayotumiwa na serikali ya Kenya kupambana na maandamano ni gharama ambazo zingeweza kutumika katika kujenga uchumi kwa hiyo ni vizuri serikali ikajikita katika kujenga uchumi kuliko kutumia gharama kubwa kukabiliana na maandamano kadharika kufanya maridhiano ili kuepusha madhara yatokanayo na maandamano,” alisema Prof Wetengere.
Kwa upande wake mchambuzi wa siasa na mambo ya kijamii Dk Faraja Kristomus alisema kukosekana kwa Maridhiano kati ya serikali na Upinzani ndio chanzo kikubwa cha madhara yote yaliyowahi kutokea huko nyuma na hata yale yatakayotokea.
"Uchumi wao uko hatarini sana, sababu kama watu hawazalishi badala yake wanafanya maandamano na uharibifu wa mali, ni wazi kwamba siku hizo tatu za maandamano zinakuja kuleta matokeo hasi zaidi na huenda likashuhudiwa anguko kubwa la Kiuchumi kuliko awali" alisema Dk Kristomus.
Dk Kristomus ambaye pia ni mhadhiri katika Chuo kikuu cha Dar es Salaam alisema kuna haja ya serikali nchini humo kusikiliza mawazo ya upinzani na kufanyia kazi hoja zao, kadharika upinzani wanapaswa kuwa wavumilivu wanapowasilisha hoja zao kusubiri zifanyiwe kazi.
Mtaalamu na mchambuzi wa siasi za maridhiano Afrika, Ezekiel Kamwaga alisema maandamano nchini humo yataendelea mpaka pale rais Ruto atakaporidhia kukaa mezani na upinzani au Kiongozi wa maandamano Odinga kuamua kusitisha maamndamano.
“Licha ya Wakenya kuwa na sababu ya maandamano ambayo ni gharama za maisha lakini Odinga ana nafasi kubwa katika maandamano hayo kwani yeye ndiye amekuwa akiitisha, kwahiyo kauli yake ina nguvu ya kuamua kuendelea au kukoma kwa maandamano,” alisema Kamwaga.
Aidha alisema maandamano hayo yanadhihirisha demokrasia iliyoko nchini humo kwani si kila taifa barani Afrika kuna uhuru wa kuandamana na kutoa maoni.