Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ruto: Niko tayari kwa mazungumzo siyo kugawana madaraka

Ruto Amuonya Odinga Dhidi Ya Maandamano Ya Umma Ruto: Niko tayari kwa mazungumzo siyo kugawana madaraka

Thu, 20 Jul 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Rais wa Kenya, Dk William Ruto, amesema yuko tayari kufanya mazungumzo kuhusu masuala yanayo waathiri Wakenya, na siyo yale yahusuyo kugawana madaraka na kiongozi wa Azimio la Umoja, Raila Odinga.

Mtandao wa Nation umelipoti leo kuwa Rais Ruto, akiwa katika Mji wa Kericho jana, alihutubia taifa katika siku ya kwanza ya maandamano ya kitaifa ya siku tatu, yakilenga kupinga ongezeko la kodi na gharama za maisha, huku akiwataka Polisi kuwashugulikia ipasavyo watu aliowaita wahalifu na wavurugaji wa amani ya nchi.

"Tuliawaambia wapinzani wetu kutushirikisha mazungumzo ya hoja zao kupitia uwakilishi wa wabunge wao, lakini wamechagua maandamano. Wanatakiwa kutumia njia zinazokubalika kisheria na kikatiba kuwasilisha madukuduku yao," amesema Rais Ruto

Ruto aliongeza kuwa uongozi wake haukinzani na vifungu vya Katiba vinavyoruhusu maandamano lakini; "Hatutakuwa Taifa la vurugu na migogoro...mtu yeyote asitutimie vifungu hivi kuchochea machafuko, sisi ni taifa la Kidemokrasia na lenye amani," alisema Ruto muda mfupi baada ya kuzindua mradi wa uzalishaji maji wa Kimugu wenye thamani ya Sh1.5 bilioni (za Kenya).

"Hatuna spare parts (vipuli) vya hili taifa letu. Ni mahala pekee tunapopaita nyumbani lazima tukubaliane kwa pamoja kupalinda na kulinda demokrasia yetu. Siasa zetu ziwe za ushindani lakini zisiwe na vurugu wala uhalifu," alisema

Wakati huo, Makamu wa Rais, Rigathi Gachagua amemshutumu Rais Mstaafu, Uhuru Kenyatta kufadhiri maandamano hayo yanayoongozwa na Odinga huku akimtaka kujitokeza hadharani kuongoza maandamano hayo ya kitaifa.

Gachagua aliutaka upinzani nchini humo kutambua kuwa uchaguzi umemalizika muda mrefu na wananchi wanatakiwa kutulia kupisha Serikali itekeleze miradi yake.

Wakati huo, Rais Ruto amesitisha uingizwaji wa vyakula na bidhaa zinazotengenezeka ndani ya nchi ili kutengeneza fursa za ajira, ubunifu na soko kwa viwanda vya ndani.

"Waagizaji wa samani kutoka nje ikiwemo viti, vitanda na meza kutoka China, Ulaya na Marekani kuanzia sasa tumesitisha....taarifa ziwafikie kwamba mkiingiza mtakutana na kodi kubwa," alisema

Rais Ruto alisema uongozi wa Jimbo la Kericho nchini humo imetenga Sh500 milioni (za Kenya) kwa ajili ya kuongeza tija katika mnyonyoro wa thamani wa mazao ya kilimo ili kukuza kipato cha wakulima nchini humo.

Ili kukuza kilimo, Ruto alitangaza kupunguza kwa pembejeo za kilimo kutoka Sh3, 500 hadi 2,500; " Tutaongeza uagizaji wa mbolea kwa ajili ya wakulima wetu kutoka magunia milioni moja za sasa hadi milioni nane kuongeza uzalishaji na kuongeza ajira nchini."

Chanzo: www.tanzaniaweb.live