Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ruto : Mvua zinazonyesha ni maombi yaliyofanywa na serikali

Ruto : Mvua Zinazonyesha Ni Maombi Yaliyofanywa Na Serikali Ruto : Mvua zinazonyesha ni maombi yaliyofanywa na serikali

Mon, 27 Nov 2023 Chanzo: Radio Jambo

Rais wa Kenya, William Ruto sasa amehusisha mvua za masika zinazoendelea kunyesha katika maeneo mengi ya humu nchini kuwa ni jibu kutokana na mkutano wa maombi ambao serikali yake iliandaa siku ya Februari 14 mapema mwaka huu katika uwanja wa Nyauo.

Akizungumza Jumapili katika ibada ya kanisa eneobunge la Roysambu, Ruto alisema kwamba kipindi hicho Kenya ilikuwa imegubikwa na kiangazi kikali kiasi kwamba baadhi ya maeneo yaliathirika kwa mifugo na binadamu kufa kwa njaa.

Baada ya kutenga Februari 14 kuwa siku ya kitaifa ya maombi, rais alisema wengi waliwacheka lakini majibu yake ndio haya.

Ruto alitangaza Februari 14 kuwa siku ya kitaifa ya kuombea taifa ili Mungu kushusha mvua.

“Tuliita mkutano tukaenda pale Nyayo Stadium tukasema tunataka kumuomba Mungu kwa sababu ya mvua, wengine wakatuchekelea wakasema angalia hawa, lakini mwaka huu tumepata mvua ajabu. Ni kweli ama si kweli?” Ruto aliwauliza waumini ambao walimpigia makofi kanisani.

Kiongozi huyo wa taifa alieleza kwamba mwaka huu kutokana na mkutano wake wa maombi, Kenya imepata mvua nyingi Zaidi kuliko jinsi ambavyo ilishuhudiwa katika kipindi cha miaka 4 iliyopita.

“Mwaka huu tumepokea mvua Zaidi kuliko ambavyo tuliwahi pokea katika miaka 4 iliyopita, kwa sababu kuomba Mungu si kazi ya mchezo, ni watu hawajui,” alisema.

Haya yanajiri wakati ambapo kumetokea mkanganyika baina ya Ruto na Naibu wake kuhusu hela za kukabili majanga ya El Nino.

Kutokana na mkanganyiko huo, Ruto anatarajiwa leo Jumatatu kuongoza kikao cha mawaziri wake ili kutafuta mwafaka kuhusu jinsi taifa litashughulikia athari za El Nino ambayo tayari mpaka sasa imeangamiza maisha ya watu wasiopungua 70.

Chanzo: Radio Jambo