Rais mteule William Ruto amewahakikishia wakenya wote kwamba hatoenda kulipiza kisasi dhidi ya wale wote waliokuwa wakimtukana na kumsimanga wakati alipotofautiana na rais anayeondoka Uhuru Kenyatta.
Akizungumza Jumatano katika mkutano na viongozi waliochaguliwa katika uchaguzi uliokamilika siku chache zilizopita, Ruto alionekana kuwazungumzia mawaziri walioegemea mrengo wa Kenyatta na kuingia katika vita vya maneno naye wakiwemo Matiang’i, Kibicho na wengine kwa kile alisema kwamba katika serikali yake, mawaziri na wafanyakazi wote katika ngazi za kiserikali hawatatumika kunadi sera au kampeni za mwanasiasa fulani bali watakuwa wanatumikia wananchi kutekeleza majukumu katika nafasi zao.
“Wafanyikazi wa umma katika serikali yangu watakuwa wataalamu, na ninategemea kwamba watawahudumia wakenya kwa njia sawa, bila kuegemea ujamaa au mirengo ya kisiasa. Wafanyikazi katika ngazi zote kuteremka chini mpaka machifu na wasaidizi wao, tutakuwa tunawategemea kuwahudumia wakenya kwa njia sawa, bila kupendelea watu kwa sababu ya mirengo yao ya kisiasa” Ruto alisema.
Akionekana kuwazushia timbwiri Matinag’i, Kibicho, Mucheru, Atwoli na mawaziri wengine ambao walijipata katikati mwa joto la kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu ambao ulikamilika wiki jana, Ruto aliwataka wote kujirudi na kufanya kazi yao kwa njia inayofaa.
“Mimi ninawauliza watumishi wote wa umma ambao walilazimishwa kuchukua misimamo katika mirengo ya kisiasa katika uchaguzi ambao umekamilika kujirudi na kufanya kazi kwa njia ya kitaalamu,” alisema Ruto.
Rais huyo mteule alisisitiza msimamo wake kwamba licha ya mambo yote aliyofanyiwa kutoka kwa baadhi ya taasisi za serikali, hawana muda kabisa wa kuenda kuzungumza kuuliza wqatu ni nini waliwafanyia na pengine kulipa kisasi.
“Tuna masuala mengi muhimu na hatuna muda kabisa wa kuzunguka kuuliza mtu eti ulisema nini, hatuna huo muda kabisa,” Ruto alisisitiza.