Raia wa Rwanda amepigwa risasi wakati wa mapigano kati ya makundi yenye silaha karibu na mpaka na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, serikali ya Rwanda imesema.
Tukio hilo lilitokea Jumatatu katika eneo la mpaka wa Rubavu, msemaji wa Rwanda Yolande Makolo alisema katika taarifa yake.
"Mwanaume aliyejeruhiwa anapokea matibabu katika Kituo cha Afya cha Cyanzarwe Rubavu," aliongeza.
Bi Makolo alisema Rwanda "ina wasiwasi mkubwa" kwa kuongezeka "kwa vitendo vya uchochezi" kwenye mpaka wake na DRC
Alivilaumu "vikundi haramu vyenye silaha vinavyoungwa mkono na Kinshasa" kwa mapigano hayo.
Msemaji huyo alisema Rwanda itadumisha "njia za kujihami na kuzuia" ili kujilinda dhidi ya ukiukaji wa anga na mipaka yake.
Hakukuwa na majibu ya haraka kutoka kwa serikali ya Congo.
Mara kwa mara Rwanda imekuwa ikiishutumu Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo kwa kushirikiana na chama cha Democratic Forces for the Liberation of Rwanda (FDLR), ambacho kinajumuisha baadhi ya watu wanaodaiwa kuwa viongozi wa mauaji ya kimbari ya Rwanda mwaka 1994. Kinshasa inapinga shutuma hizo.
Kwa upande wake, DRC inaishutumu Rwanda kwa kuunga mkono wanamgambo wa M23 - kundi la waasi wa kabila la Watutsi wa Congo - madai ambayo Kigali inakanusha.