Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ripoti: Watoto milioni 333 duniani kote wanaishi katika ufukara

Njaaaa Ripoti: Watoto milioni 333 duniani kote wanaishi katika ufukara

Thu, 14 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ripoti mpya iliyotolewa Jumatano kwa pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF na Benki ya Dunia inasema zaidi ya watoto milioni 333 duniani kote wanaishi katika ufukara, huku kudorora uchumi kulikochangiwa na janga la COVID-19 kwa miaka mitatu kukichochea zaidi janga hilo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo mtoto 1 kati ya 6 kote duniani anaishi kwa chini ya dola 2 na senti 15 kwa siku ikiwa imepungua kutoka watoto milioni 383 hadi milioni 333 sawa na asilimia 13 kati ya mwaka 2013 na 2022.

Ripoti imesema athari za kiuchumi za janga la COVID-19 zimechangia kupotea kwa miaka mitatu ya kupiga hatua za kiuchumi na kuwaacha watoto milioni 30 zaidi kusalia katika umasikini ambao walitarajiwa kuondolewa kwenye jinamizi hilo.

Tathimini hii iliyotolewa kuelekea mjadala wa Baraza Kuu la umoja wa Mataifa wa ngazi ya juu wiki ijayo ambao pamoja na mambo mengine viongozi wa dunia watathimini hatua za mchakato wa utekelezaji wa malengo ya malengo ya maendeleo endelevu SDG’s inaonya kwamba lengo la kutokomeza umasikini kwa watoto ifikapo mwaka 2030 halitotimia.

Mkurugenzi mtendaji wa UNICEF Catherine Russell amesema "Miaka saba iliyopita, dunia ilitoa ahadi ya kumaliza umaskini uliokithiri kwa watoto ifikapo mwaka 2030. Tumepiga hatua, tukionyesha kwamba kwa uwekezaji na utashi sahihi, kuna uwezekano wa kuwainua mamilioni ya watoto kutoka katika hali mbaya ya maisha ya umaskini."

Naye Luis-Felipe Lopez-Calva mkurugenzi wa kimataifa wa Benki ya Dunia wa masuala ya umaskini na usawa amesema "Dunia ambapo watoto milioni 333 wanaishi katika umaskini uliokithiri na kunyimwa sio tu mahitaji ya msingi lakini pia utu, fursa au matumaini hali hii haiwezi kuvumiliwa.

Tathimini ya ripoti hiyo inaonyesha kuwa nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ndizo zinazobeba mzigo mkubwa zaidi wa watoto masikini kwani asilimia 40 wanaishi katika ufukara, na ilichangia ongezeko kubwa la Watoto masikini katika muongo uliopita, ikipanda kutoka asilimia 54.8 mwaka 2013 hadi asilimia 71.1 mwaka 2022.

Wakati huo huo, ripoti inasema maeneo mengine yote duniani yameshuhudia kupungua kwa kasi kwa viwango vya umaskini uliokithiri, isipokuwa Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live