Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa alitangaza mabadiliko ya Baraza la Mawaziri Jumatatu usiku, na kumteua naibu rais mpya na mawaziri kadhaa.
"Nimeamua kumteua Bw. Paul Mashatile kama naibu rais wa jamhuri," Ramaphosa amesema katika hotuba yake kwa njia ya televisheni.
Anachukua nafasi ya David Mabuza, ambaye alijiuzulu mwezi uliopita.
Mashatile, 61, pia anahudumu kama naibu rais wa chama tawala cha African National Congress (ANC).
Ramaphosa pia ameanzisha wizara mbili, ikiwamo ya umeme na nyingine ya Mipango, Ufuatiliaji na Tathmini ambayo itazingatia zaidi utendaji wa serikali.
Amemteua Kgosientsho Ramokgopa kama waziri katika Afisi ya Urais anayesghulikia umeme. Sasa atakuwa na jukumu la kusuluhisha mzozo wa sasa wa umeme unaokabili nchi hiyo yenye uchumi mkubwa zaidi wa kiviwanda barani Afrika.
Afrika Kusini inakabiliwa na tatizo kubwa zaidi la umeme kuwahi kutokea katika miongo kadhaa, huku umeme ukiwa unakatika mara kwa mara hadi saa sita kwa siku.
"Kazi ya msingi ya waziri mpya itakuwa kupunguza kwa kiasi kikubwa uhaba wa umeme kama jambo la dharura," kiongozi huyo wa Afrika Kusini amesema.
Ramaphosa amesema waziri wa umeme atatarajiwa kuratibu idara na taasisi zote zinazohusika katika kukabiliana na mgogoro huo, ikiwa ni pamoja na kufanya kazi na uongozi wa shirika la umeme la Eskom kwa ajili ya kuongeza kasi ya uzalishaji umeme kwa njia mpya.