Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ramaphosa aapishwa kuwa rais wa Afrika Kusini kwa muhula wa pili

ANC Kampeni Ramaphosa.png Ramaphosa aapishwa kuwa rais wa Afrika Kusini kwa muhula wa pili

Wed, 19 Jun 2024 Chanzo: Bbc

Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini ameapishwa kwa muhula wa pili wa urais, licha ya kushindwa kupata wabunge wengi katika uchaguzi wa mwezi uliopita wa chama chake cha African National Congress (ANC).

Wabunge walimchagua tena kuwa rais wiki iliyopita kufuatia makubaliano kati ya ANC, mpinzani wake wa muda mrefu wa Democratic Alliance (DA) na vyama vingine kuunda serikali ya mseto.

Chama cha ANC, ambacho kimetawala tangu mwisho wa ubaguzi wa rangi mwaka 1994, kilipoteza wingi wa viti vya ubunge kwa mara ya kwanza baada ya uchaguzi wa Mei 29 kutotoa mshindi wa moja kwa moja.

Viongozi wengi wakiwemo wakuu kadhaa wa mataifa ya Afrika wanahudhuria sherehe hizo.

"Ninaapa nitakuwa mwaminifu kwa Jamhuri ya Afrika Kusini...nitatii, nitazingatia katiba na sheria nyingine zote za jamhuri," Bw Ramaphosa alisema.

Kiapo hicho kilisimamiwa na Jaji Mkuu Raymond Zondo.

Baada ya Bw Ramaphosa kula kiapo, bendi iliimba wimbo wa taifa uliofuatwa na salamu ya bunduki 21 na kuruka kwa helikopta za jeshi, kabla ya kutoa hotuba yake ya kuapishwa.

Chama cha uMkhonto weSizwe (MK) kilichoundwa miezi sita iliyopita na Rais wa zamani Jacob Zuma kinasema maafisa wake hawatashiriki katika uapisho wa "kifahari".

Chama hicho, ambacho kilipata 15% ya kura na kupata viti 58 vya ubunge, pia kilisusia kikao cha kwanza cha bunge Ijumaa iliyopita.

Chanzo: Bbc